January 13, 2017Katika hali isiyokuwa ya kawaida, timu ya wanawake ya mchezo wa soka ya Victoria Queens ya Kagera imepokwa pointi baada ya kushindwa kufika kituoni Kigoma kucheza mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake dhidi ya Sisters FC kutokana na ukata.

Uongozi wa Victoria umethibitisha juu ya suala hilo na kudai kuwa licha ya kuomba msaada kwa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA) ambacho mwenyekiti wake ni Jamal Malinzi, bado walikwama na hivyo kushindwa kusafiri.

Kocha Mkuu wa Victoria Queens, George Simon alisema wamesikitishwa na hali hiyo kwa kuwa haikuwa dhamira yao.

"Kiukweli timu imeshindwa kusafiri baada ya nauli kukosekana kwani hatuna mdhamini ndiyo maana imetukuta hali hiyo na tumejaribu kutafuta msaada tumekosa," alisema Simon.

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa KRFA, Saloum Chama alithibitisha kwa kusema: "Ni kweli timu yetu ya Victoria imeshindwa kusafiri baada ya kukosa nauli, sisi chama tumeshindwa kuisaidia kwani hatuna ruzuku kutoka popote na hatuna pia vyanzo vya mapato vya kuiwezesha timu yetu kusafiri hivyo tumekwama kwa njia hiyo."

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Kigoma (KFA), Omary Gindi alisema, Sister FC ilifuata taratibu zote na imejipatia pointi tatu za mezani kutokana na wapinzani wao kutofika uwanjani.
"Wametuogopa tu, kwani kwao tuliwafunga mabao 9-0 wangekuja kwetu ingekuwaje?" alihoji Gindi.


Ikumbukwe kuwa, Malinzi pia ndiye Rais wa Shirisho la Soka la Tanzania (TFF) na amekuwa mstari wa mbele kupigania soka la wanawake lakini timu ya mkoa anaouongoza imepata ‘majanga’.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV