January 25, 2017



Na Saleh Ally
MKUU wa Kitengo cha Habari cha Klabu ya Simba, Haji Sunday Manara juzi ameandika waraka wake akielezea namna ambavyo anaamini Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa si makini katika suala la ratiba.
Moja ya sehemu ya alichoandika Manara katika makala yake hiyo ni hiki hapa;


“Wakati wenzetu wanazungumzia  changamoto nzito na kubwa katika maendeleo yao ya mchezo murua zaidi duniani wa soka. Watanzania tunahangaika namna ya kupanga ratiba ya mechi zetu za ligi yetu na Kombe la Shirikisho, ratiba inayobadilishwa Kama nguo, tena mvaaji mwenyewe ni mbunifu wa mavazi au mwanamitindo, ambae huvaa nguo tano Kwa siku.”


Mwishoni alimalizia hivi: “Nimalizie Kwa kuwapa mtihani mwingine TFF na bodi ya Ligi, iwapo kama ratiba yao ya ligi kuu na Kombe la Shirikisho haitabadilishwa kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu, ntamposa mlimbwende Wema Sepetu, na akikubali ntamuoa. Akikataa ntatembea na boxer (nguo ya ndani) tokea nyumbani kwangu hadi TFF.”


Umbali wa kutoka nyumbani kwa Manara, Magomeni Mikumi hadi TFF si mbali sana, takribani kilomita tatu au nne. Kweli si mbali lakini kwa kutembea na nguo ya ndani, hata hatua nne ukiwa hadharani, ni mbali sana.


Jiulize kwa nini Manara anaweza kutoa kauli tata kama hiyo ya kumposa au kumuoa Wema Sepetu au kutembea na nguo ya ndani huku akijiamini haiwezi kutokea.


Haiwezi kutokea na ana uhakika kwa kuwa anaijua TFF kwamba si ya uhakika na mambo yao mengi ni ya kubahatisha. Kwa hiyo uhakika unapozungumzia mambo yasiyo na uhakikia, kwa TFF ni uhakika.


Lakini unapozungumzia yale ya uhakika kwa TFF si uhakika. Ndiyo maana Manara anaweza kutoa ahadi ambayo anajua ni ngumu kwake lakini ana uhakika hawezi kuifanya kwa kuwa TFF haitaweza kwenda mwendo sahihi.


Kweli, kama watu wanazungumzia mambo ya maendeleo mengi, vipi sisi hadi leo eti ratiba haiwezi kupangwa bila ya kuwa na mabadiliko?


TFF inawezaje kuzungumzia program bora ya vijana kwa muda mfupi na mrefu au ya soka la wanawake kwa muda mfupi na mrefu wakati ratiba ya msimu mmoja tu haina uhakika wa kuipanga ikiwa na uhakika?


Kumekuwa na mawazo ya kuongeza watu uwanjani baada ya mapato kuathirika kwa kiasi kikubwa na suala la mechi kuanza kuonyeshwa mujarabu na runinga ya Azam TV.

Moja ya mikakati ilikuwa ni kuzungumzia uuzaji wa tiketi kwa msimu au nusu msimu. Lakini unawezaje kufanya hivyo wakati hakuna uhakika wa ratiba?

TFF hiyohiyo, ilifanya madudu msimu uliopita kwa kuiruhusu Azam FC iondoke kwenda kucheza mechi za tamasha nchini Zambia na kusababisha kuwe na viporo kwenye ligi kuu.
Baada ya presha kubwa ya vyombo vya habari, nayo ikaweka presha kwa Azam FC kuhakikisha inamaliza viporo vyote baada ya kurejea kwenye ligi kuu. Ukiangalia hapa, hakukuwa na sababu za msingi na TFF yenyewe ilionyesha haiheshimu ratiba ya ligi ambayo imepangwa na wanaoitwa wataalamu.


Ligi inakwenda na malalamiko makubwa ya viwango duni vya waamuzi, viwango duni vya upangaji ratiba lakini hata viwanja vibovu ambalo liko nje ya TFF. Kwa nini TFF isiwe mstari wa mbele kuondoa mapungufu hayo laini ya upande wake ambayo yanawezekana?

Binafsi siamini kama kuna kiongozi hata mmoja wa shirikisho hilo anataka maendeleo ya soka nchini. Ninaamini hivi; viongozi wanataka maendeleo yao, ya familia zao, ya ndugu zao na ikiwezekana ya washikaji wao tena si kwenye mpira.


Umesikia siku nne tu zimepita, eti waliopanga ratiba ya Kombe la Shirikisho ambalo TFF wanadhaminiwa na Azam Sports HD kwa mamilioni ya fedha. Lakini eti wapanga ratiba waliisahau timu.


Kwangu niliona kama miujiza, lakini miujiza ya TFF haijawahi kupungua kwa kuwa kila mwaka inaongezeka. Hivyo kushangaa ni kujishangaza tu maana pale ndiyo jumba la miujiza.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic