January 16, 2017

MTIBWA SUGAR MSIMU ULIOPITA, KIKOSI CHAO HAPA KIKIWA NA KICHUYA, MUZAMIRU NA MO IBRAHIM AMBAO SASA NI TEGEMEO SIMBA.



Wababe wa Morogoro, Mtibwa Sugar, hawana hofu hata kidogo. Wanasema wapinzani wao Simba wasifikirie kutwaa pointi tatu kutoka kwao kwa kuwa wanaijua vyema safu yao ya ushambuliaji ambayo ni zao lao, akiwemo Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahimu ‘Mo’, Mzamiru Yassin na Juma Luizio, kwa kuwa ni wachezaji waliowalea wenyewe na wanatambua upungufu wao.

Simba na Mtibwa zinatarajiwa kukutana keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, baada ya ligi kusimama kwa muda kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyomalizika Ijumaa iliyopita huku Azam ikitwaa ubingwa huo.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisema wanaiheshimu Simba kwa kuwa ni timu inayoongoza msimamo wa ligi na ipo vizuri lakini wasitegemee kuwafunga katika uwanja wao wa nyumbani, kwa kuwa wanaijua vilivyo safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kutokana na asilimia kubwa ya wachezaji wao wote, wametokea Mtibwa, hivyo wanazifahamu mbinu zao.

“Tuko vizuri kukabiliana na Simba kuelekea mchezo wetu wa Jumatano kwani kipindi hiki cha mapumziko mafupi ya wiki mbili, kimetusaidia, tumefanya mazoezi makali ambayo yametusaidia kukiimarisha kikosi.

“Lengo letu ni kuhakikisha hatufungwi katika mechi zetu zilizobakia katika mzunguko wa pili kwani kuna ushindani mkubwa kwa kuwa kila timu inahitaji kushinda na sisi hatujapoteza mchezo wetu hata mmoja, hivyo Simba wasitarajie kupata pointi tatu hapa kwetu.

“Hatuihofii safu ya ushambuliaji ya Simba kwani tunaifahamu vyema safu yote ya ushambuliaji kwa kuwa wote wametoka Mtibwa Sugar na tumewalea wenyewe na tunatambua vizuri mbinu zao, hivyo hazitupi shida. 

“Wachezaji wetu wana morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huo, japokuwa tunaiheshimu Simba kwa kuwa inaongoza msimamo, tunahitaji kushinda katika uwanja wetu wa nyumbani kwa kushirikiana na mashabiki wetu ambao watatupa sapoti kubwa,” alisema Kifaru.

Mtibwa itaingia kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 30, wakati Simba ipo kileleni na pointi 44.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic