January 16, 2017




Na Saleh Ally
AZAM FC iliyokuwa inakwenda kwa mwendo wa kusuasua, imekwenda na kuamka katika michuano ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuibuka mabingwa.

Kikosi cha Azam FC chini ya aliyekuwa kocha wa muda, Iddi Cheche, beki wa zamani wa Sigara, kimefanikiwa kubeba kombe hilo bila ya kupoteza mchezo wala kufungwa hata bao moja.



Unaweza kusema Azam imeibuka na ubingwa ikiwa na rekodi ya asilimia mia ya ubora tofauti na mwendo wake katika Ligi Kuu Bara.

Azam FC imemaliza Ligi Kuu Bara mzunguko wa kwanza ikiwa katika nafasi ya tatu. Sasa kama ilivyo kwa timu nyingine nyingi imecheza mechi tatu za mzunguko wa pili.

Ilikuwa chini ya Kocha Zeben Hernandez raia wa Hispania ambaye yeye na jopo lake walitimuliwa siku moja kabla ya Azam FC haijacheza mechi ya tatu ya mzunguko wa pili dhidi ya Prisons na kushinda kwa mara ya kwanza katika mzunguko huo kwa bao 1-0.

Zeben na wenzake waliishuhudia Azam FC ikishinda mechi hiyo huku wao wakiwa wameiongoza katika mzunguko huo kwa mechi mbili na zote zilikuwa sare dhidi ya Lyon (0-0) na Majimaji (1-1).

Ndani ya mechi tatu, Azam FC ilikusanya pointi tano, maana yake imepoteza nne. Tofauti na Yanga na Simba ambao mwendo wao si mbaya sana, hapa sasa ni Ligi Kuu Bara.

Vinara Simba, ambao waliingia fainali ya Mapinduzi na kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC, wamekusanya pointi tisa katika mechi zote tatu huku Yanga wakiwa wamepata alama saba baada ya sare moja na ushindi mara mbili.

Kama ni takwimu za mechi tatu zilizopita kwa kila timu kati ya hizo tatu za juu, Simba ambao wanaongoza wakiwa na pointi 44, wanaonekana wana mwendo mzuri wa ukusanyaji wa pointi. Wanafuatiwa na Yanga wenye pointi 40, ingawa hawa wanaonekana uwezo wao wa kufunga uko juu sana.

Yanga wamekusanya pointi saba lakini katika mechi hizo tatu wamefunga mabao nane, Simba wamefunga manne na Azam FC mawili.

Kwa upande wa difensi, katika mechi hizo tatu, Simba haijaruhusu bao hata moja wakati Yanga na Azam kila moja imeruhusu bao moja. Utaona ingawa Simba haijaruhusu, lakini hakuna tofauti kubwa kwa maana ya safu ngumu za ulinzi.

Hii ni hali ya tahadhari kwa Simba, lakini Azam FC pia ambao ufungaji wao unaonekana kusua ukilinganisha na Yanga. Hii pia inaonyesha namna gani ligi inaweza kuwa ngumu na kila timu lazima ibadilishe ile hali ya kuamini.



Simba hawapaswi kulala usingizi na kuamini uchezaji wao wa mechi tatu zilizopita kwa kuwa Mapinduzi itakuwa imewakumbusha jambo. Yanga pia kwamba wametolewa nusu fainali lakini si sababu ya kuona walifeli na kurudisha presha kwenye ligi.

Azam FC wanaweza kuitumia hali ya morali kurejea vizuri kwenye ligi kuu ingawa hakuna ubishi lazima wafanye kazi kubwa ya kuisahau sherehe ya kombe hilo na kurejea kweli kwenye ligi.

Ligi na michuano “Tournaments” ni vitu vinavyopishana kabisa. Hata aina yake ya upangaji wa mambo unakuwa tofauti kabisa. Hivyo, michuano ya Mapinduzi inaweza kuwa imeisaidia Azam FC kuangalia mambo iliyokuwa inakosea ingawa unaweza kuwa mtihani upya kwa maana sasa wakati inarudi kwenye ligi, itaanza na kocha mpya Aristica Cioaba kutoka Romania.

Hii ni patapotea nyingine kwa Azam FC, kwani kama kocha Cioaba atafanikiwa kuendeleza moto wa kina Cheche, itakuwa vizuri, lakini akiingiza mifumo mingi mipya kwa wakati mmoja, itakuwa rahisi kuwachanganya wachezaji wake na mwisho, watarudi kama ilivyokuwa mzunguko wa kwanza.

Azam FC ina kila sababu ya kubadilika na kuendelea kwa kiwango cha juu kwa kuwa ikiwa Zanzibar imewafunga vigogo wa Visiwani na vigogo wa Bara hadi ikatwaa ubingwa.


Yote yawepo lakini vizuri kutofautisha ligi na tournament, ni mambo mawili yenye mfumo na mwendo tofauti, kitaalamu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic