January 14, 2017Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, imeanzisha rasmi vita kwa wanamichezo na viongozi wa michezo mbalimbali ambao wamekuwa wakihusika na dawa za kuongeza nguvu michezoni.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa tume ya taifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sanaa na Utamaduni (Unesco), Dk. Moshi Kimizi katika semina ya siku moja ya udhibiti wa dawa hizo.

Kimizi alisema Tanzania imesaini mkataba maalum na Chama cha Kuzuia Dawa Haramu Michezoni Duniani (Wada), hivyo ina wajibu wa kuhakikisha wanamichezo wake wanajihepusha nazo ili kuficha aibu ya taifa.“Semina hii ya siku moja itasaidia kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wa michezo katika kusaidia upigaji vita matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni ambazo zinasababisha matokeo yasiyo halali.

“Kwa kushirikiana na wizara husika ya michezo, tunaamini tutafanikiwa kupiga vita dawa hizo na hatutoweza kuvumilia kuona vipaji vya wachezaji wetu vinapotea kwa sababu ya madawa ya kuongeza nguvu michezoni.“Na hii itasaidia kuficha heshima ya taifa, chama husika na mchezaji pale itapogundulika mchezaji anatumia dawa hizo mara baada ya kushinda mashindano atakayoshindana,” alisema Kimizi.

Mkufunzi katika semina hiyo, Dk. Henry Tandau alisema kuwa vita dhidi ya matumizi ya dawa hizo, siyo nyepesi na inahitaji nguvu za pamoja kukomesha.


“Matumizi ya dawa hizi ni biashara kubwa ambayo mtu mmoja au watu wachache hawawezi kuidhibiti. Ni vigumu kwa mtu wa kawaida kufanya hivyo kwani hufanyikia kwenye maabara ambazo humilikiwa na watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha,” alisema Tandau.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV