January 16, 2017



Na Saleh Ally
WAKATI fulani niliwahi kuandika juu ya uamuzi wa Yanga kuhusu makocha wawili, George Lwandamina raia wa Zambia na Hans van Der Pluijm kubaki pamoja kuwa si sawa.

Niliamini si sawa kwa kuwa makocha hao wawili wote unaweza kusema ni wa kiwango kinachofanana na wanabaki pamoja baada ya kuonekana Yanga inahitaji mtu wa kuiendeleza zaidi.

Yanga inataka kufanya vizuri zaidi kimataifa na Lwandamina akiwa na Zesco ya kwao Zambia alifanikiwa kufanya vizuri na kufika nusu fainali, wakatolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo baadaye ikachukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Uamuzi wa Yanga kumtoa Pluijm ni kwamba inataka mtu wa kuiendeleza tokea hapo. Lakini si sawa, mtu huyo kuendelea kubaki na akawa bosi wa yule mpya ambaye anatakiwa kusukuma gurudumu. Ushauri wangu ukawa hivi; Yanga ichague kubaki na mmoja.

Wakati nikiwa nimeshauri hivyo, hivi karibuni nimekuwa nikisikia mambo mengi sana ambayo yanahusiana na Lwandamina na Pluijm na mara nyingi utayasikia Yanga inaposhinda au kupoteza.

Kila inaposhinda, Yanga wamekuwa wakilazimika kufananisha kwamba Lwandamina ni hatari na Yanga inacheza kwa kasi kubwa na haikamatiki.


Lakini inapotokea Yanga imepoteza, basi utasikia “bora babu Pluijm, huyu Lwandamina anatuzingua tu”. Kwa lugha nyepesi hii unaweza kusema Yanga wamekuwa wakijishambulia wenyewe kila wakati kwa kuwa kumsakama au kumkandia mmoja kati ya makocha hao ni kujishambulia tu.

Kilichonisikitisha zaidi ni baada ya kugundua hata baadhi ya viongozi wa Yanga walio ndani ya klabu hiyo nao wako kwenye makundi katika suala la makocha hao wawili.

Najua kila kitu kinafanyika kwa siri kubwa, lakini kuna wale wasiokubaliana na Pluijm ambaye huenda awali hakufurahishwa na jambo lao fulani na sasa wanaona ni wakati wa kuona hana nafasi katika kila kitu.

Lakini wako wanaoona Pluijm ni poa sana kwa kuwa ndiye amekuwa akifanya kazi nao vizuri. Hili linakwenda hadi kwa wachezaji wenyewe kwamba wanaona Pluijm ni bora zaidi.
Hakuna anayeweza kukubali, lakini kama makocha hawa wawili wataendelea kubaki pamoja baadaye hakutakuwa na ubishi.

Ukweli ukiwekwa hata ndani ya maji, ukandamize na majabali, nakuhakikishia itafika siku utatoka na nafasi ya kuuzuia haitakuwepo hata kidogo.

Ndani ya Klabu ya Yanga, kuna viongozi wengi vijana ambao ukiangalia uamuzi wa klabu hiyo unalenga zaidi kutaka kuwasaidia kuwafundisha ili kuhakikisha wanakuwa viongozi imara baadaye.

Utakuwa na elimu nzuri kutoka chuo, hiyo bado haiwezi kuwa sababu ya kukupa ubora, badala yake unatakiwa kufanya mambo kwa vitendo. Cheti pekee hakiwezi kukamilisha kuwa mtendaji anayeweza kuwa bora.

Ninaamini Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji analijua hilo, ndiyo maana anataka kujitahidi kuwafunza ili baadaye wawe msaada mkubwa katika klabu hiyo.
Lakini ninachokiona, wako ambao hawajui Yanga inataka nini na inawezekana ndani ya muda mfupi sana wamejiona ni bora kabisa, hawataki tena kufundishwa na bila wao kujua “wameanza kutia maji ndani ya mtumbwi”.

Kiongozi bora hawezi kuendekeza ushabiki, kiongozi anayetaka ubora hawezi kujifunza kwa kuwashambulia wengine ndani ya anachokiongoza, badala yake anatakiwa kuwa na machaguo matatu, moja; kuwafunza, pili kuwapa nafasi waendelee kujifunza na tatu kukubali waende na kuchukua nafasi nyingine.


Kama anaamua kuwa ndani ya klabu kama kiongozi, hakuna ujanja ni lazima aipiganie klabu yake, la sivyo, atakuwa ni kiongozi anayeangalia kushibisha tumbo lake na yupo kwenye klabu kwa ajili ya maslahi yake binafsi na si maendeleo ya anachokiongoza na jina sahihi kwake ni “kiongozi dhaifu, asiyefaa”.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic