January 23, 2017



Yanga imetamba kuwa hawataliacha taji lao la ubingwa wa Kombe la FA wanalolitetea na badala yake watapambana vya kutosha kuhakikisha wanaubakiza ubingwa huo.

Kauli hiyo, ilitolewa na Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi mara baada ya mechi ya Kombe la FA iliyowakutanisha na Ashanti United mchezo uliomalizika kwa Yanga kushinda mabao 4-1.

Katika mechi hiyo, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam Yanga iliingia uwanjani bila ya nyota wake wanne Kelvin Yondani (majeruhi), Deogratius Munishi 'Dida', Donald Ngoma (wote wenye matatizo ya kifamilia), Nadir Haroub 'Cannavaro' (malaria) na Hassani Kessy (Typhoid).

Mwambusi amesema kamwe hawataidharau timu yoyote watakayokutana nayo kwenye michuano hiyo mikubwa ili kuhakikisha wanalitetea kombe lao.

Mwambusi alisema, wamecheza mechi na Ashanti bila ya kufanya maandalizi ya kutosha na hiyo imetokana na kubanwa na ratiba ambayo ilitoka siku moja kabla ya mechi hiyo.

Aliongeza kuwa, anawapongeza wachezaji wake kwa kiwango kikubwa walichokionyesha, licha kutopata muda wa kupumzika wakitoka Songea kucheza na Majimaji kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo Yanga walishinda bao 1-0 lililofungwa na Deus Kaseke.

"Kwanza kabisa nianze kwa kuwapongeza wachezaji wetu kwa kuonyesha kiwango kikubwa licha ya kuchoka na safari ya Songea tulipokwenda kucheza mechi ya ligi kuu na Majimaji ambayo tulishinda.

"Ushindi huo tulioupata tuliutarajia kutokana na mikakati tuliyoipanga kwenye timu yetu ambayo ni lazima tulitetea kombe letu la FA tulilolichukua, mwaka jana na tuliingia uwanjani katika mechi hiyo kwa lengo la kupata ushindi ambao tumeupata.


"Na kikubwa tulichokipanga ni kutodharau timu yoyote tutakayocheza nayo, kama unavyojua FA inashirikisha timu za Ligi Daraja la Kwanza, hivyo hatutaidharau timu yoyote ikiwemo hii ya ligi kuu na Ligi Daraja la Kwanza," alisema Mwambusi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic