January 23, 2017Beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Joshua, amewashangaza makocha wake kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani kitendo ambacho kimemfanya kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi, kusema huyo ndiye kiraka wao kwa sasa baada ya kuondoka kwa Mnyarwanda, Mbuyu Twite.

Mwambusi ametoa kauli hiyo baada ya Joshua ambaye kiuhalisia ni beki wa kushoto, siku za hivi karibuni kwenye mechi tofauti kuanza kutumikia nafasi nyingine uwanjani kama kiungo, beki wa kati  'kisasa' na straika.

Juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar, wakati Yanga ilipoifunga Ashanti United mabao 4-1 katika mchezo wa Kombe la FA, Joshua alicheza beki wa kati sambamba na Andrew Vicent ‘Dante’.

“Katika mchezo huu, ameonekana anahitajika kucheza nafasi aliyocheza na tunashukuru amecheza vizuri na kuziba pengo la yule mwenye nafasi yake, tunampongeza kwa uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi uwanjani na kufuata maelekezo tunayompa, tunaweza kusema huyu ndiye kiraka wetu kwa sasa,” alisema Mwambusi. 

Ikumbukwe kuwa, tangu Yanga imlete Mzambia George Lwandamina kuwa kocha mkuu huku ikiachana na Twite aliyetimkia Fanja ya Oman, Joshua amekuwa akicheza nafasi tofauti na ile iliyozoeleka.


Mara ya kwanza kwenye Kombe la Mapinduzi lililomalizika hivi karibuni visiwani Zanzibar, katika mchezo dhidi ya Zimamoto, alichezeshwa mshambuliaji alipoingia kuchukua nafasi ya Juma Mahadhi, kisha katika Ligi Kuu Bara dhidi ya Majimaji, akaingia kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima na kucheza kiungo wa kati kabla ya juzi kucheza beki wa kati akichukua nafasi ya Kelvin Yondani ambaye alikosekana kwenye mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV