June 28, 2017
Na Saleh Ally
UNAWEZA kusema sasa mwonekano wa michuano ya Mabara maarufu kama Confederation Cup sasa umefikia patamu hasa.

Michuano hiyo imefikia hatua ya nusu fainali ambayo ni hakika kumbashiri bingwa ni nani lakini haitakuwa mchezo kwa kuwa kila timu kati ya nne zilizoingia nusu fainali inaonekana ni hatari.

Angalia wenyeji Russia, wameshindwa kufikia hatua hiyo, maana katika Kundi A, Ureno na Mexico ndiyo wamefuzu na Kundi B waliofuzu ni Ujerumani na Chile.

Mashabiki wa Tanzania wanakuwa na raha kwa kuwa michuano hiyo inarushwa moja kwa moja katika king’amuzi cha StarTimes na kazi ya nusu fainali inaanza leo wakati Ureno inayoongozwa na Cristiano Ronaldo itakapokuwa na kazi ngumu dhidi ya Chile chini Alexis Sanchez, pia usisahau mtu kama Arturo Vidal.

Ukiangalia kabla ya kutinga nusu fainali, Chile ilishinda 2-0 dhidi ya Cameroon halafu ikapata sare mbili za 1-1 dhidi ya Ujerumani na Australia, hivyo si timu ya kubeza na inaonekana kuwa na difensi ngumu. Au unaweza kusema, ukibeti umeliwa, maana haujui nani anashinda.

Ureno wao ndiyo vinara wa Kundi A, Ronaldo akiwa ndiye chachu na wanaonekana kuwa hatari zaidi. Licha ya kuanza kwa sare ya 2-2 dhidi ya Mexico waliamka na kushinda 1-0 dhidi ya wenyeji Russia kabla ya kuwashindilia New Zealand kwa mabao 4-0.

Nusu fainali ni mtoano, unaweza ukawa bora katika makundi, ukizubaa hatua hiyo umekwenda. Hata kama utawala Ureno asilimia 65-35 lakini bado wanapaswa kuwa makini kwa kuwa Chile ina watu zaidi ya watatu wanaoweza kuamua matokeo nje ya mfumo wa kocha.

Raha nyingine kwa wanaoshuhudia michuano hiyo kupitia king’amuzi cha StarTimes ni hivi; mechi ya pili ni kesho wakati vinara wa Kundi B Ujerumani watakapowavaa Mexico.

Ujerumani ina mabadiliko makubwa katika kikosi wakionekana kujipanga kwa ajili ya Kombe la Dunia 2018. Lakini kikosi kinaonekana imara zaidi kwani katika mechi tatu za makundi wamefunga mabao saba, si mchezo.

Ujerumani ilianza kwa kuitwanga Australia 3-2, ikarudi na kupata sare ya 1-1 dhidi ya Chile kabla ya kuishinda Cameroon 3-1.

Udhaifu unaoonekana ni kwamba pamoja na Ujerumani kuwa na safu kali ya ushambulizi inayoongozwa na Lars Stindl, bado ulinzi wake si imara kwa kuwa ndani ya mechi tatu umeruhusu mabao manne au umefungwa kila mechi.

Mexico nao si wa kubeza, Ujerumani wanapaswa kuwa makini kwa kuwa walikomaa na Ureno mechi za Kundi A na kutoka nao sare ya 2-2. Hawachoki na wapiganaji hasa.

Usimsahau Javier Hernandez ‘Chicharito’, anacheza Ujerumani na anakutana na Wajerumani lakini ni mtu mwenye njaa hasa ya mabao. Hivyo itakuwa mechi nyingine yenye presha dakika ya kwanza hadi 90.

Utaona Mexico wana uwezo mzuri pia wa kufunga, katika mechi tatu wamefunga mabao sita, mawili kila mechi. Hivyo, wamecheza mechi tatu kila moja wakifunga mawili. Ujerumani inabidi wajipange kuwazuia wasiendeleze rekodi yao.


Mechi hizo za leo na kesho, ni burudani tosha kwa wapenda soka na uzuri nyota wa timu za La Liga, Premier League, Bundesliga na ligi nyingine maarufu watakuwa wanachuana vikali. Si mechi za kuzikosa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV