June 28, 2017





Na Saleh Ally
INGAWA kusomea muhimu lakini suala la biashara pia ni kipaji na mshambuliaji mpya tena wa Simba, Emmanuel Okwi anaweza kuwa mfano wa watu wenye vipaji vya biashara.

Okwi ana uwezo mkubwa wa kuifanya biashara yake kwa ubunifu mkubwa na mwisho akawaacha wateja au wahusika anaofanya nao biashara wakiwa na furaha kubwa na yeye akiendelea kutengeneza fedha.

Kwanza, ni mtu wa kuthubutu na haoni shida kufanya biashara anapoona kuna biashara. Si mwoga na haogopi kuvunja biashara anapoona hakuna biashara.

Kwa hapa nyumbani, wafanyabiashara wanaojulikana kwa kujitolea na kutaka kufanikisha wanachotaka ni ndugu zetu wa kabila la Wachaga. Hawa huanza na duka dogo hadi linakua na baadaye wakawa matajiri, hawahofii kujaribu na si watu wa kukata tamaa, ndiyo maana wamekuwa mfano.
Kwa Okwi, kujitolea bila ya woga si jambo kubwa kwake, maana yake ni kujaribu ambalo wengine wangehofia. Ndani ya kipaji cha Okwi, inaonyesha hilo ni sehemu kubwa ya alichonacho na wengi hawana. Maana hata hao Wachaga huenda ‘wanamshangaa’.

Juzi amerejea Simba kwa mara ya tatu tokea alipojiunga nayo mwaka 2009 kwa mara kwanza akitokea SC Club Villa ya Uganda akiwa kinda mwenye miaka 17 tu. Furaha ni kubwa kwa mashabiki wa Simba lakini faraja ni kubwa kwa kuwa Okwi, yeye ameingiza mamilioni ya fedha.

Simba imemwaga dola 50,000 (zaidi ya Sh milioni 110) ambazo zote ameweka kibindoni kwa kuwa mjadala wake na Simba haukuwa na wakala pia hakuwa na mkataba na SC Villa ambayo imekuwa kituo kila anapotoka nje, anarejea hapo.

Hesabu za haraka zinaonyesha tangu mwaka 2009, Okwi alipotokea SC Villa hadi leo, amehama mara nane katika nchi za Uganda, Tanzania, Tunisia na Denmark na ametengeneza kiasi kikubwa cha fedha.

Lakini pamoja na kutengeneza fedha hizo, Okwi ameisaidia Simba kutengeneza fedha nyingi na kumfanya kuwa mchezaji aliyeipatia Simba faida kubwa kuliko mwingine yeyote.



Simba ilimnunua kwa dola 20,000 (zaidi ya Sh milioni 40) akitokea SC Villa, nayo ikamuuza Etoile du Sahel ya Tunisia kwa kitita cha dola 300,000 (zaidi ya Sh milioni 660).

Tunisia Okwi hakudumu, akavunja mkataba na kurejea SC Villa ambako aliweza kuweka kituo hadi aliponunuliwa na Yanga kwa dola 35,000 (zaidi ya Sh milioni 77) ambako hakudumu pia hadi alipoamua kurejea Simba akiwa huru na kusajiliwa kwa dola 20,000 tena.

Simba ilikaa naye na ndani ya msimu ilishapata biashara na kumuuza Sonderjysker ya Denmark kwa kitita cha dola 100,000 (zaidi ya Sh milioni 221). Huko nako hakudumu, akarejea SC Villa na kuweka kituo ambao wao walimpa dola 5,000 (zaidi ya Sh milioni 11) kama walivyofanya mwanzo wakati anatua akitokea Etoile.

Taarifa zinaeleza Okwi huwa haingii mkataba na Villa lakini kama atapata timu nyingine, huwarudishia dola 5,000 yao na ziada kidogo kama timu yake iliyomlea na inayompokea anapokuwa amevunja mkataba sehemu.

Sasa ametua Simba na kuchota kitita hicho cha dola 50,000 akiwa anakamilisha kuhama mara nane tokea 2009. Kila uhamisho akiwa ameingiza fedha na pia kaiingizia Simba dola 400,000 (zaidi Sh milioni 884).



Simba imegharimika dola takribani 100,000 kumnasa mara zote tatu alizojiunga nayo. Mara moja 20,000 halafu 20,000 tena na 50,000 lakini kuna fedha ambazo hutoka katika ukamilishaji wa mikataba.

Hivyo, Simba ndiyo imepata faida zaidi kwa kuwa inaonekana faida yake kwa Okwi ni dola 300,000.

Utaona namna Okwi anavyoweza kucheza na “mapengo” ya kutengeneza biashara wakati anatoka timu moja kwenda nyingine. Lakini angalia alivyo mjanja pale anapovunja mkataba na timu moja, haraka anakuwa huru na anaporejea Villa anapiga soka kweli na kutengeneza kiwango.

Anapopata timu, basi anakuwa na nafasi ya kuchota dau kubwa. Anawagawia Villa kidogo anakwenda kupiga kazi. Baada ya msimu mmoja, mwisho miwili lazima atapata soko na ikishindikana anavunja mkataba.



Hata hivyo inaonekana hivi, amevunja mkataba kutoka timu zenye fedha nyingi kama zile za Ulaya na Amerika Kusini. Na kutoka katika timu ambazo hazina uwezo mkubwa sana, huko anajituma na kupata soko la kuuzwa.

Okwi anakuwa uwanjani lakini anajua anachokifanya kwa ajili ya ‘ku-market’ au unaweza kusema hivi; Okwi ni Ofisa Masoko wa Okwi”.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic