July 7, 2017


Na Saleh Ally
UKIONA mwenyeji wako anakukaribisha halafu anakueleza jambo kuonyesha ana hofu nawe kuhusiana na jambo fulani basi ujue una shida hiyo na unapaswa kuirekebisha mapema.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa amemkaribisha mshambuliaji mpya wa Yanga, Ibrahim Ajibu kwa bashasha lakini akawa mkweli na kumueleza wazi ambacho alikifikiria.

Pamoja na maneno mengi yaliyoonyesha kumkaribisha Ajibu, Mkwasa alikuwa wazi kwa kumtaka kujituma na kushikilia suala la nidhamu kuwa ni muhimu sana.

Kauli ya Mkwasa unaweza kuichukulia juujuu lakini ukifanya hivyo utakuwa umesahau kuwa Mkwasa ni kocha na alikuwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars.

Wakati akiwa kocha mkuu, mara kadhaa alimuita Ajibu, alikaa naye kambini na nikukumbushe anajua mambo mengi ya Ajibu anapokuwa uwanjani au nje, hivyo alikuwa akizungumza huku akimaanisha.

Hakuna anayefanikiwa katika soka kwa kuwa na uwezo wa kucheza pekee. Wapo wengi wenye uwezo wa kucheza mpira leo bado wanacheza mechi za Uswahilini huko mchangani na wanaofanana kiuwezo nao wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya wakilipwa mamilioni ya fedha kwa wiki.

Tofauti yao kubwa ni nidhamu tu na leo nalikumbushia hili kama ambavyo niliwahi kuelezea hili tena wakati Ajibu akiwa Simba baada ya Msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara kusema baada ya wasanii wawili maarufu, mburudishaji mwingine nchini ni Ibrahim Ajibu pekee.

Nilimkumbusha kuhusiana na nidhamu, nikamkumbusha kuhusiana na malengo na kumsisitiza Ajibu anatakiwa kusaidia timu kupata mafanikio na kutoa matokeo na si kuburudisha kwa kupiga chenga nyingi uwanjani.

Kujiunga kwake Yanga, akakaribishwa kwa tahadhari lazima ajiulize na kubadilika ili kipaji chake na uamuzi wake wa kwenda Yanga uwe sahihi.

1. ASIOGOPE
Ajibu hapaswi kuwa na hofu hata kidogo kuhusiana na uamuzi wake wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kuwa mpira ni kazi yake. Watu wengi hasa mashabiki wa soka ni “selfish” au wabinafsi na wanaotaka kuburudishwa wao bila kujali mburudishaji anaishi vipi.

Kazi ya Ajibu ni mpira, kama kapata dau kubwa vipi abaki kwa sababu ya mapenzi tu. Kikubwa anapambana ili akue, hivyo kama kaamua kwenda Yanga basi ajiamini na kufanya kazi yake kwa kuwa hajafanya uamuzi mbaya.

 2. HAJAKOSEA YANGA
Hakuna anayeweza kumuambia amekosea, ukiacha ushabiki, Ajibu anaonekana amepiga hesabu sawasawa kwa kuwa amejiunga na mabingwa wa nchi, timu itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wakati akivishwa jezi ya Yanga, alionekana hajiamini au ni mtu mwenye kuona jambo fulani si sawa. Maisha yanakwenda na mabadiliko na unapoyafanya lazima ujiamini na kuyasimamia. Kama akiteleza Yanga, safari ya kuyumba itaanza, hivyo ni lazima kuamini uamuzi aliochukua ni sahihi.

Hivyo anapaswa kuamini ni uamuzi sahihi na anachotakiwa ni kujituma ili kufikia malengo.

3. AACHE UTOTO
Watanzania wengi si watu wanaoweza kusema ukweli na wangependa kusema jambo litakalomfurahisha Ajibu. Mimi nasema ukweli, Ajibu akichukia atakuwa ameshajifunza. Aache utoto.

Wakati anakuzwa Simba ilikuwa ni rahisi kusema ana utoto lakini sasa ni wakati wa kuonyesha uwezo wake alionao kwa kuisaidia timu anayoitumikia. Simba wakati wanaamua kukaa kimya wakimdengulia walitumia kigezo cha hakuwa na msaada na timu.

Ukiangalia uwezo wake na takwimu za msaada kwa maana amefunga mabao mangapi, pasi ngapi za mabao na kadhalika utaona yuko chini sana na chenga ndiyo nyingi na bahati mbaya hazihesabiki kitaalamu. Hivyo ni lazima abadilike na kuwa mchezaji sahihi mwenye msaada chanya kusaidia kupatikana kwa ushindi na kuzalisha pointi. Kama ni chenga, ziwe “chenga zalishi”.

4. MALENGO LAZIMA
Ajibu ametua Yanga, kaingia katika rekodi ya wachezaji waliocheza Simba na Yanga au waliohama kutoka timu moja kwenda nyingine wakiwa nyota tayari.

Sasa baada ya hapo anataka nini? Arudi kucheza Simba tena au ajiunge na Azam FC au Singida United? Huu ni wakati mwafaka wa yeye kuitumia nafasi ya Yanga na ushiriki wake wa michuano ya kimataifa kwenda mbele zaidi.

Ajibu anatakiwa kwenda kucheza nje ya Tanzania. Aitumikie Yanga kwa juhudi kubwa ili kutimiza ndoto ya mchezaji mwenye malengo sahihi. Tayari kafanya majaribio Misri, akafeli. Kufeli ni kujifunza na sasa anatakiwa kutengeneza  nafasi nyingine ya majaribio.

5. AWAACHE MASHABIKI
Akitaka kufanikiwa zaidi hana sababu ya kushindana na mashabiki ambao amewaacha, hasa wale wa Simba la sivyo watampoteza.

Mashabiki nao wana nguvu yao na wangependa kumchanganya. Inakuwa rahisi kujichanganya hasa unapoona mtu aliyekuwa anakuunga mkono, anakugeuka na kukuzomea.

Hapo shabiki anakuwa anafanya kazi yake ya kuisaidia timu yake, hivyo Ajibu naye afanye kazi yake maana maneno yao hayawezi kumtoboa.

6. ASIKATE TAMAA
Hakuna njia ya maisha isiyokuwa na mabonde, lazima Ajibu ataipitia akiwa Yanga kama alivyokuwa Simba na katika maisha ya kawaida.

Kama itatokea anatakiwa kuipitia akipambana kutatua tatizo, hapaswi kujuta na kufikiri alikosea. Matatizo ni kila sehemu na ujasiri ni jambo jema kwa kuwa sisi Watanzania ni watu wa maneno mengi, hivyo Ajibu asiungane na maneno, apige kazi.

7. LAZIMA AIPENDE YANGA
Nimeona watu wengi wakifanikiwa kwa kupenda wanachokitumikia. Mimi naipenda ofisi ninayoitumikia na kama gazeti la michezo, utanieleza nini kuhusu CHAMPIONI?
Kama unalipenda gazeti jingine na unafanya CHAMPIONI utakuwa ukatuni. Na Ajibu akicheza Yanga eti huku anaipenda sana Simba kuliko Yanga, utakuwa ni zaidi ya ukatuni.

Kazi yako inayokulipa mshahara, inayoendesha maisha yako na unaitumia kuendesha ndoto zako halafu izidiwe na mapenzi ya furaha tu, huu ni ushabiki wa kijinga na vizuri wakaachiwa wanaoshabikia kuliko wanaotumikia.

Maisha yanabadilika na Ajibu hana ujanja, anapaswa kuipenda Yanga ili afanye vizuri zaidi akiwa anaitumikia maana unachokipenda hautafurahia kuona kinafeli hadi kuanguka na kikifanikiwa, wewe unakuwa umefanikiwa pia.




2 COMMENTS:

  1. Aende na aoneshe Simba no chuo cha wachezaji bora na so bora wachezaji!

    ReplyDelete
  2. Aende na aoneshe Simba ni chuo cha wachezaji bora na si bora wachezaji!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic