July 1, 2017
Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Everton ndiyo pekee kutoka England itasafiri barani Afrika kwa ajili ya maandalizi yake ya msimu mpya wa Premier League na nchi itakayofanya maandalizi hayo ni Tanzania.

Arsenal watakuwa Shanghai, China, Chelsea watasafiri hadi nchini Singapore huku kikosi cha Manchester United chini ya Jose Mourinho kikipaa kutoka England hadi Houston na baadaye Los Angeles nchini Marekani.

Everton watasafiri Kilomita 4,836 kutoka jijini Liverpool hadi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maandalizi hayo ya msimu mpya na watacheza na mabingwa wa SportPesa Super Cup, Gor Mahia.

Mechi hiyo itapigwa Julai 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku mashabiki wa soka nchini na wale wa nchi jirani wakiwa na shauku kubwa kuwaona moja kwa moja uwanjani nyota wa Everton kama vile Ross Barkley, Aaron Lenon, Leighton Baines na wengine wengi ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiwatazama kwenye runinga.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Everton, Robert Elstone alikuwa nchini na alitangaza rasmi ujio huo wa Everton. Akiwa nchini aliongozana na balozi wa klabu hiyo, Leon Osman.

Osman ni mmoja wa magwiji wa soka nchini England na amecheza mechi za kutosha akiwa na Everton zinazomfanya kuingia katika rekodi ya wakongwe.Osman ambaye ameichezea Klabu ya Everton zaidi ya mechi 400 kabla ya kustaafu mwaka 2016, alipata fursa ya kuonana na vijana kutoka kwenye shule nne za soka jijini Dar es Salaam za Bombom FC, EFCA Academy, TIMAD Academy, JKYP Academy na kuzungumza nao masuala kadhaa kuhusiana na uzoefu wake katika soka kwa miaka zaidi ya 17 ambayo amecheza.

“Huo ulikuwa ni mwanzo tu kuelekea kwenye ujio kamili wa Everton mwezi ujao wa Julai ambapo pia wachezaji vijana kutoka klabu za Simba, Yanga, Singida United na timu ya taifa ya vijana tutawaona.

“Lakini kutakuwa na fursa ya kukutana na makocha kutoka Everton na kufanya nao mazoezi ikiwa ni moja ya program nyingi ambazo zitafanyika siku za tarehe 12 na 13 katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),” anasema.

“Vijana ndiyo msingi sahihi wa kutengeneza ubora wa soka. Kuna kila sababu ya kuwapa nafasi kwa kuwakuza zaidi katika misingi sahihi. Tanzania ina vipaji na kikubwa ni kuendelea kutoa mafunzo sahihi kwao na walimu ambao watakuwa sahihi kuwafundisha,” anaongeza.Osman alizungumzia jinsi ambavyo safari ya soka ilivyo ndefu na wala siyo jambo la kuamka siku moja na kufanikiwa huku akiamini kuwa kama njia hizo za malezi ya soka kwa vijana zitazingatiwa kwa ufasaha, basi nchi za Afrika hasa Tanzania zina nafasi ya kufanya vizuri kwenye soka la kiushindani miaka michache ijayo.

“Unajua aina ya ubora unaotakiwa kuuonyesha katika ngazi ya juu ya kimataifa haiji ndani ya siku moja kwani huchukua miaka mingi ya maendeleo na unatakiwa kuanza na vijana wadogo na baada ya miaka kumi unaanza kuona matunda yao yakijitokeza hivyo ninajua kwa hakika kuwa nchi za Afrika zitatoa ushindani mkubwa zaidi miaka michache ijayo lakini kama nilivyosema ili kufikia hatua hiyo, unatakiwa kuanza mapema zaidi.”

Mbali na uvumilivu katika kukuza vipaji vichanga, Osman pia alisisitiza kuhusu suala zima la wachezaji hawa chipukizi kuwa na bidii katika kutimiza malengo yao na pia kuzingatia nidhamu ili waweze kuwa bora zaidi ndani na nje ya uwanja.“Unatakiwa uwe na lengo la dhati juu ya kile unachotaka kufanikiwa, inaweza kuwa mpira wa miguu au kitu chochote kwenye maisha ambacho utachagua na unatakiwa kuwa na shauku ya kukitaka na kukipata. Pia unatakiwa kuwa na nidhamu katika kutimiza ndoto yako bila kujali nini kinajitokeza njiani, kiwe kizuri au kibaya lakini usikate tamaa na endelea kuamini katika ndoto zako.”Osman alimalizia kwa kuwaambia wachezaji wa kitanzania wenye ndoto za kucheza EPL kuwa siyo rahisi hata kidogo kucheza kwenye ligi na inatakiwa uwe mchezaji mzuri hasa huku akisisitiza kuwa ili kuweza kuwa na kiwango hicho ni lazima uanze kucheza katika ngazi za chini.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV