July 7, 2017

Baba mzazi wa kipa wa Simba, Peter Manyika, Manyika Peter ameibuka na kuwaambia viongozi wa timu hiyo kuwa kama wanataka mtoto wake abaki Msimbazi, basi awe anapata nafasi ya kucheza asilimia 99.9.

Lakini taarifa nyingine zinathibitisha kuwa Manyika ameamua mwanaye aondoke Simba kwa kuwa hana nafasi ya kucheza.

Kauli hiyo, ameitoa ikiwa ni siku chache timu hiyo ifanikiwe kunasa saini ya kipa namba moja wa Taifa Stars, Aishi Manula.Manula amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba akitokea Azam FC akiwa mchezaji huru.

Akizungumza na Spoti Hausi kupitia Global TV Online, Peter alisema akiwa kama meneja wa kipa huyo, anataka kuona mchezaji wake akipata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza kutokana na sifa alizonazo.

Baba huyo alisema kipa huyo ana ndoto kubwa wa kucheza soka la kimataifa ambalo anaamini kama akiendelea kubaki Simba bila ya kupata nafasi ya kucheza, basi kiwango chake kitashuka, hivyo ni bora akamuondoa na kwenda kucheza soka kwingine.

“Ninaongea kama meneja wa mchezaji hivi sasa siyo mwanangu, sitaki kumuona akiendelea kuichezea Simba kwenye misimu mingine mara baada ya mkataba wake huu kumalizika.

“Na nitamuondoa kutokana na kutopewa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, hivyo kama kweli Simba wanamhitaji basi wamtumie katika kikosi cha kwanza kwa asilimia 99.9.

“Ukiangalia Peter ni kipa mzuri na umri wake ni mdogo, hivyo nikikubali kumuacha aendelee kukaa benchi ni kama ninafurahia kuona kipaji chake kikishuka,” alisema Manyika.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV