July 8, 2017Baada ya kiungo wa Simba, Mzamiru Yassin kuwavutia mawakala mbalimbali nchini Afrika Kusini, uongozi wa klabu hiyo umesema unasubiri ofa zije ili wamuuze mchezaji huyo.

Mzamiru ambaye yupo Afrika Kusini na kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa), baada ya kuonyesha kiwango kizuri ameripotiwa kuzivutia timu za Bidvest Wits na Mpumalanga Black Aces za nchini humo.

Kutokana na hali hiyo, Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Idd Kajuna, amesema hakuna ofa waliyopokea lakini ikija wataishughulikia haraka, hivyo kama kweli amewavutia wanapaswa kupeleka ofa yao.

“Kufanya vizuri uwanjani kwa Mzamiru hiyo ni kawaida yake, kama kuna timu zilimuona amefanya vizuri na zikavutiwa naye zinatakiwa kufuata utaratibu wa kuwasiliana nasi.

“Kwa sasa hatuwezi kusema sana kwa sababu hakuna hata timu iliyotuambia inamtaka Mzamiru, lakini kama itatokea basi tutazungumza nao,” alisema Kajuna.


Wakati huohuo, Mzamiru akizungumza kutoka Afrika Kusini, alisema: “Hayo mambo kila siku yanasemwa ila mimi sijafuatwa bado, kama wananitaka wawasiliane na Simba kwa hatua zaidi.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV