Na Saleh Ally
SIMBA ilifanikiwa kufika katika hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la SportPesa Super Cup iliyokuwa inafanyika nchini Kenya.
Katika fainali hiyo, Simba ililala kwa mabao 2-0 na kuwaacha Gor Mahia wakiendelea kuchukua ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Msimu uliopita ikiwa ndiyo mara ya kwanza michuano hiyo inaanzishwa, Gor Mahia ilibeba kombe katika ardhi ya Tanzania, ikiwachapa wapinzani wao wakubwa AFC Leopards kwa mabao 3-0.
Fainali zilicheza timu za Kenya pekee, mwisho zikawa na uhakika wa kucheza na Everton ya England. BAadaye mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Watanzania na aibu zetu, tukaenda uwanjani kushuhudia nyasi zetu zikiumizwa na wageni.
Safari hii, Wakenya waliamini biashara itaendelea na wao kukutana katika hatua ya fainali. Hasa ukizingatia siku ya kwanza ya mashindano, Yanga ilifungwa mabao 3-1 na Kakamega Homeboyz na kutolewa na Gor Mahia, ikaing’oa JKU kwa mabao 3-0.
Ikawa siku mbaya kwa Watanzania na ikaonekana itaendelea. Siku ya pili, Simba na Singida United zikavuka kwenda nusu fainali na kutengeneza nusu Tanzania na nusu Kenya.
Ukikiangalia kikosi cha Simba, kilikosa wachezaji wengi muhimu ambao kama wangekuwa na kikosi chao kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kubeba ubingwa huo.
Ubingwa huo fedha zake ni dola 30,000 (zaidi ya Sh….), kama haitoshi bingwa anasafiri kwenda England kucheza na Everton FC kwenye Uwanja wa Goodison Park jijini Liverpool.
Simba ilikwenda na kikosi ambacho hakika kama kingekuwa hivyo kisingechukua ubingwa. Lakini nyota wengi walionekana wazi waliamua kubaki Dar es Salaam au kwingine kwa kuwa waliyachukulia mashindano hayo kama vile hayakuwa na faida yoyote kwao na kwa klabu.
Msimu uliopita, mashindano ya SportPesa Super Cup, Yanga na Simba waliamua kujaribu wachezaji na mwisho wakatia aibu kupindukia.
Safari hii, walionekana kubadilika kidogo, lakini uimara wa viongozi kuonyesha wanatambua umuhimu wake ukawa chini na baadhi ya wachezaji wakawa na nguvu zaidi.
Mfano, mchezaji kama Said Hamis Ndemla ambaye sasa anakua kisoka, aliamua kubaki Dar es Salaam sababu imeelezwa kwamba mkataba wake na Simba uliisha.
Ndemla alibaki hadi hapo atakapomalizana na Simba. Naweza kusema ni sawa, lakini bado nakuwa na mawazo tofauti kwa kuwa naona huenda wiki moja ya michuano hiyo isingedhuru Ndemla kuisaidia Simba na pia kujisaidia yeye binafsi, nitaeleza.
Kama Simba ingeshinda michuano hiyo maana yake wanaokwenda mmoja wapo ni Ndemla. Maana yake, Ndemla angepata uzoefu zaidi kucheza michuano hiyo lakini nafasi ya kucheza England dhidi ya Everton kwenye Uwanja wa Goodison Park, si kitu kidogo.
Sasa kama alibaki Dar es Salaam na kucheza mechi za kirafiki, Simba imepoteza na mwisho wakiingia mkataba na kukubaliana, maana yake Simba na yeye walipoteza muhimu ambayo wangeweza kuipigania kwa shida na baadaye mambo yakikaa vizuri wanakuwa kitu mkononi.
Wakati Simba ilimkosa Haruna Niyonzima katika fainali, basi kama ingekuwa na Ndemla, isingeyumba na ingeweza kuwa na nafasi ya kufanya vizuri na kuwapa shida kubwa Gor Mahia ambao zaidi walijisifia wachezaji wakongwe ambao hakika waliifanya kazi yao vizuri.
Shiza Kichuya naye alifanya hivyo, mwisho baada ya kumalizana na uongozi akasafiir kwenda Kenya na mwisho akacheza kwa kiwango cha chini kabisa. Kwa kifupi hakuwa na msaada mkubwa kama uwezo wake ulivyo na inaonekana kisaikolojia hakuwa ameelekeza nguvu katika michuano hiyo.
Angalia Emmanuel Okwi, mfungaji bora wa Simba ambaye pia aliona ni wakati mzuri wa kupumzika na familia wakati timu yake ikipambana ile mbaya kuhakikisha inalinda heshima na kupata kitu kikubwa ambacho huenda ni bora kuliko hata michuano ya Kagame.
Bora Simba wangewekeza nguvu nyingi katika michuano hiyo ya SportPesa Super Cup na baada ya hapo wangepumzisha wachezaji wakati wa Kagame.
Sitaki kuwabana wachezaji kwamba wasidai haki zao, lakini ninawakumbusha na kuwasisitiza lazima wasijione kama wanaitumikia Simba kuisaidia, au mafanikio ya Simba ni ya klabu na wao hawafanikiwi na lolote.
Wachezaji wanapaswa kukumbuka, uhusiano wao na Simba haupaswi kujengwa na fedha pekee. Upendo utakapoingia katikati, kuna wakati mambo yanaweza kwenda na kuwa mazuri hata bila ya fedha kwa kuwa fedha haiwezi kuzidi nguvu ya upendo.
Ninaamini, timu za Kenya zitafanya hivyo. Zitapumzisha wachezaji wake wakati wa Kombe la Kagame baada ya kuwa zimepambana vilivyo katika Super Cup ya SportPesa.
Wakenya ni wajanja, wanajua kipi ni muhimu zaidi. Lakini sisi tunafanya mambo kwa mazoea. Huenda itaendelea hivi kwa miaka kadhaa na siku tutakapofuambua macho, Wakenya watakuwa wametumia nafasi hiyo muhimu kwa miaka mingi na kujitangaza sana.
Ninaamini, kucheza tu England, wachezaji hao wa Kenya watajitangaza kwa kiasi kikubwa na kuna uwezekano kupata nafasi ya kutoka na kwenda kucheza hata katika nchi nyingine za Ulaya.
Mawakala watakaposikia timu kutoka Afrika inakwenda kucheza na Everton, lazima watataka kuona hiyo timu na wachezaji wake na kuangalia kama wanaweza kufanya biashara.
Lakini hapa nyumbani, bado mambo ni ya kubahatisha. Hakika nakuwa tofauti na watu wengi nikiamini, kama Simba na Yanga zingeenda zikiwa na vikosi vyao sahihi, basi kulikuwa na uwezekano kukutana fainali au moja kuingia na kuchukua ubingwa.
Angalia Gor Mahia, inakutana na Simba inayoksoa safu yote kali ya ushambulizi. Lakini imeifunga bao 2-0. Kama ingekuwa na ubora wa juu, basi ingeshinda 5-0.
Kikubwa cha kuangalia na kujifunza kwa wachezaji wa Kenya ni uelewa, kujitambua na wanajua wanataka nini. Watanzania tunaendelea kubaki na vipaji bora lakini tusiojitambua na viongozi wenye hofu ya kuwaudhi wachezaji.
Umeongea brother ukweli mtupu lakini ulioyaongea ni kupoteza muda wako kwani inaonekana kama sisi watanzania ni fungu la kukosa. Siku moja nilianza kutoa maoni yangu kwa kuanza sisi watanzania ni watu wa hovyo basi nilinyanganyiliwa kama mpira wa kona watu wakitaka kumalizia hasira zao kwa vitendo kwenye miwili wangu. Lakini ukweli ni ukweli hata ukibisha utabakia kuwa ukweli na hata sisi wenyewe tukijipumbaza kuupuzia ukweli basi zaidi ni kuwapa watu wengine nafasi kuona kuwa sisi ni watu wa hovyo. Hovyo sio tusi bali ni hali ya mtu kutokuwa na uwezo wa kujitambua wakati ana akili zake timu kwa kufanya mambo ya kukirihisha.
ReplyDeleteKuna neno wanasema like father like son hali ya kurisishana tabia hasa mbaya kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.Tulitarajia kizazi hiki kipya kuwa na mitizamo chanya zaidi kwani madhumuni makubwa kabisa ya uwepo wa tv ni kutoa elimu pana zaidi ya Dunia kitu amabacho wazee wetu waliikosa nafasi hiyo na kama vile haitoshi kukaongezeka mambo ya internet ili watu wawe na wigo mpana zaidi wa kujifunza mambo mbali mbali lakini inaonekana sisi Watanzania baada ya kutumia vitu hivi kwa kujitafutia maendeleo tunavitumia kujitafutia ujinga.
Wenzetu wazungi zamani sana tena sana walitambua kuwa maisha ni vita bila ya kujitolea kwa akili na kimwili basi yakutawala na kubakia mtumwa wa maisha kila siku. Ile nafasi ya Sport pesa piga ua ilikuwa si ya kuifanyia mzaha hata kidogo kwa timu zetu. Kijana kama Manula hakika ni wakati wa kupata nafasi wa kuonyesha uwezo wake nje ya nchi. Ili kuwa na timu imara ya taifa lazima tulazimishe kupeleka vijana wetu nje ya nchi hilo jambo kamwe hatutakiwi kumsubiri mtu kuja kuwaondosha vijana wetu kwani bado hatujawa na mazingira yeyote yale ya kuwafanya watu wa nje kuja kuchukua wachezaji wetu.