October 17, 2018



MOJA ya wachezaji ambao wanaaminika kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa kwenye soka duniani ni Kylian Mbappe ambaye anaichezea PSG ya Ufaransa.
 

Mshambuliaji huyo ameshaonyesha mambo mengi makubwa kwenye ulimwengu wa soka kwa sasa akiwa ameshafanya vizuri kwenye timu ya taifa ya Ufaransa.
 


Kwenye fainali za Kombe la Dunia alikuwa mmoja kati ya wachezaji walioisaidia sana timu hiyo kutwaa ubingwa wa kombe hilo kwa kuifungia mabao manne likiwemo moja kwenye mchezo wa fainali.

Wengi wanaamini kuwa kijana huyo msimu huu ndiyo ataonyesha kiwango cha juu zaidi kuliko kipindi kingine kilichopita kutokana na umri wake.


Mbappe ambaye alijiunga na PSG akitokea Monaco kwa mkopo msimu huu ameshaonyesha cheche zake akiwa anashika nafasi ya kwanza kwa kupachika mabao kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa, Ligue 1, baada ya kufunga mara nane.


Kiwango chake kimeonekana kukua kwa kasi ya hali ya juu kwa kuwa msimu mzima uliopita alifanikiwa kufunga mabao 13 tu.


Katika michezo mitano ya Ligi Kuu ya Ufaransa aliyocheza ametoa asisiti tatu na hivyo amehusika kwenye mabao 11 ya timu yake hadi sasa.
Mbappe ambaye anaaminikia kuwa ana kasi nzuri uwanjani
amekuwa akishirikiana kwa karibu na Neymar ambaye naye ameshapachika idadi hiyo ya mabao wavuni.


“Tumeanza msimu vizuri sana, naona kama tunaweza kufanya vizuri kwa sasa kuliko msimu uliopita, pamoja na mambo mengine ni vizuri kama tunaweza kufanya mambo makubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwenye ligi.


“Ushirikiano kama timu ndiyo pekee unaweza kutufanya tukapata mafanikio uwanjani, lazima tukubali kuwa ligi ni ngumu na kila mmoja anataka kuona timu yake inapata mafanikio uwanjani,” alisema Mbappe.


Hata hivyo, doa kwa mchezaji huyo msimu huu ni kwamba hadi sasa ameshapewa kadi moja nyekundu wakati msimu uliopita aliumaliza akiwa hana kadi hata moja nyekundu.
Katika michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo mchezaji huyo amecheza hadi sasa amefanikiwa kufunga mabao mawili akionekana kuwa anaweza kufanya vizuri huku kuliko misimu mingine.


Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19, kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizopita
alitangazwa kama mchezaji bora kijana dalili zikiwa zinaonyesha kuwa anaweza kuwika zaidi kwa siku kadhaa mbele.


Katika maisha yake ya soka, msimu wa 2016/ 2017, ndiyo alipata mafanikio makubwa zaidi ambapo alimaliza msimu akiwa na Monaco kwa kufunga mabao 26.


Inaaminika kuwa msimu huu anaweza kufanya vizuri kuliko msimu huo kutokana na kasi nzuri ambayo ameanza nayo, lakini pia akiwa anawania tuzo ya mchezaji bora wa dunia, ballor d’or.


Mbappe ambaye baba yake ni Mcameroon na mama yake raia wa Algeria mwanzoni mwa msimu huu alisema kuwa anataka kuona anafunga kuanzia mabao 20 na zaidi kwenye ligi kuu.
“Tunaye Neymar kwa sasa na wachezaji wengine wengi wapo vizuri kikosini, naamini kuwa tunaweza kufanya vizuri zaidi ya misimu iliyopita.


“Ninachotaka kuona ni kufunga mabao zaidi ya 20 msimu huu, hiki ndiyo kinaweza kuwa kitu bora zaidi kwangu,” alisema mchezaji huyo ambaye ameshaifungia Ufaransa mabao 10 kwenye michezo 25 aliyocheza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic