December 15, 2018


Nahodha wa Taifa Stars na klabu ya KRC Genk, Mbwana Samatta amefunguka juu ya historia ya maisha yake ya soka kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi katika klabu hiyo.

Alipokuwa akifanya mahojiano na mtandao wa Klabu ya Genk, Samatta amesema kuwa alianza kucheza soka tangu alipokuwa mtaani Jijini Dar es Salaam ambapo katika kipindi hicho alishindwa hata kumudu kununua jozi ya kiatu cha kuchezea.

Ameendelea kusema kuwa kwenye nchi nyingi za Afrika hasa Tanzania hakuna ‘Academy’ za kuweza kuwaandaa vijana kucheza soka kwa ubora na kutimiza ndoto zao za maisha kama ilivyo kwa mabara mengine, isipokuwa kwa juhudi binafsi ambazo wachezaji wachache ndio wanaoweza kufanya hivyo.

Kuhusu mazingira ya soka nchini Tanzania na mchezaji gani ambaye yeye anamuiga na anayetamani kufanana naye (Role model), Samatta amesema, “Mashabiki wengi wa soka nchini Tanzania wanapenda sana kutazama EPL na mimi nilikuwa mmoja wao, pindi nilipokuwa nikimtazama Thierry Henry nlikuwa najisemea mwenyewe ‘ nataka kuwa kama huyu’, ni kama role model ambaye amenishawishi sana“.

“Nilitamani sana kipindi hicho kuja siku moja kucheza soka barani Ulaya kwasababu ni kitu ambacho nilikuwa ninakitazama kupitia televisheni, ndiyo maana nilipopata nafasi ya kuja hapa wala sikusita,” ameongeza Samatta.

Usiku wa jana, umeshuhudiwa nahodha huyo wa Taifa Stars, Mbwana Samatta na klabu yake ya KRC Genk wakifuzu hatua ya 32 bora ya michuano ya Europa League baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Sarpsborg na kumaliza kundi wakiwa vinara wa kundi lao la ‘L’.

Pia katika ligi ya Ubelgiji ‘First Division A’, Genk inaongoza msimamo kwa alama 39 baada ya kushinda mechi 11, ikitoa sare 6 na kupoteza mchezo mmoja mpaka sasa na kuwaacha wapinzani wao Royal Antwerp wanaoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama 4.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic