January 20, 2019


Wanachama waandamizi wa Yanga pamoja na baadhi ya viongozi wamesisitiza kwamba kuna haja ya kipa namba moja wa timu hiyo, Beno Kakolanya kurejeshwa kikosini.

Kiwango cha kipa Mkongomani Klaus Kindoki kwenye mechi ya jana pamoja na zile za hivi karibuni kimewatisha wadau hao kuelekea mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Lakini Kocha Mwinyi Zahera amewaambia kwamba; “Beno wakala wake ndiye aliyeomba kuvunja mkataba na sisi tukamkubalia, mpaka sasa iko hivyo hakuna mabadiliko.”

Yanga jana Jumamosi ilichapwa bao 1-0 na Stand United mjini Shinyanga na kutibua rekodi yao ya kutopoteza mechi tangu msimu huu uanze.

Kipa mahiri wa zamani wa Yanga Manyika Peter ambaye pia ni mwanachama wa timu hiyo alisema; “Bado kuna uhitaji wa Yanga kufanya maboresho hasa kwa mlinda mlango kutokana na nafasi hiyo kuwa muhimu, Kindoki anafanya makosa ya mara kwa mara hali ambayo inafanya ashindwe kuisaidia timu hivyo kuna haja ya kufanya utafiti kwa timu aliyotoka kujua makosa yake.

“Beno Kakolanya nilipata nafasi ya kuwa naye kwenye timu ya taifa na alianza kuwa kwenye ubora wake hivyo ni mtu mwenye uwezo wa kuisaidia Yanga endapo atapata nafasi ya kucheza, kikubwa ni umakini hasa kwenye safu ya mlinda mlango.”

Staa mwenye rekodi ndani ya Yanga, Edibily Lunyamila alisema; “Pengo la Beno Kakolanya Yanga linaonekana wazi kwani makipa wote waliokuwepo hawawezi kumfikia kiwango chake anayedaka na anayekaa benchi hawana tofauti. Kikosi kwa ujumla sio kibaya isipokuwa nafasi ya kipa ndio tatizo.”

Hashim Abdallah, Mjumbe mwenye ushawishi ndani ya kamati ya Utendaji Yanga alisema; “Kwa makipa ambao wapo Yanga kwa kwa sasa Kakolanya ana nafasi kubwa tu kwa hasa ukiangalia suala la uwezo. Beno anastahili kucheza Yanga.”

Meneja wa Kakolanya, Seleman Haroub amefunguka kuwa mwenye jibu la kuwa Beno Kakolanya kasemehewa au la ni kocha Zahera pekee yeye hana taarifa yoyote.

“Lakini katika kulinda kipaji cha nyota huyo kwa sasa anafanya mazoezi binafsi ili kuendelea kuwa bora kama ilivyo kwa siku zote,” alisema meneja huyo.

Alipotafutwa Kakolanya alisema kwa kifupi: “Nimeambiwa na meneja wangu nisizungumze chochote kuhusiana na suala hilo.”

Tathmini kiufundi inaonyesha kwamba Kakolanya amecheza mechi sita msimu huu huku akipigwa mabao sita. Ramadhani Kabwili amecheza mechi 8 akapigwa bao saba huku Kakolanya akicheza nane na kufungwa mawili.

1 COMMENTS:

  1. Aende Zake.
    Nidhamu ni Bora Na Kipaji Bila Nidhamu ni Kazi Bure Muulize Balotelli

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic