April 18, 2019


HATIMAYE juhudi za Simba kwenye michuano ya kimataifa zimezaa matunda ambapo sasa kuanzia msimu wa 2020-21, Tanzania itakuwa inaingiza timu nne kimataifa.

Simba walikuwa wakishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo walitolewa kwenye hatua ya robo fainali baada ya kuchapwa mabao 4-1 na TP Mazembe nchini Congo, wikiendi iliyopita.

Hata hivyo, nafasi hiyo imeisaidia Tanzania ambapo sasa kwa mara ya kwanza itakuwa na nafasi nne kwenye michuano ya kimataifa, Kombe la Shirikisho zitaingia timu mbili na Ligi ya Mabingwa Afrika timu mbili.

Hii ni kuanzia msimu wa 2020-21. Kwa mujibu wa Msemaji wa Caf, Mamadou Gaye, ambaye Championi lilimfungia safari na kuzungumza naye, alisema uwezo ambao Simba wameuonyesha,
umewasaidia kupata pointi nyingi ambazo zimeweza kuifanya Tanzania kuwa nafasi ya 12 kwenye msimamo na hivyo wanaongozewa nafasi mbili.

Msemaji huyo amesema kuwa Tanzania kwa sasa inashika nafasi ya 12 na kiwango cha mwisho cha timu kupewa nafasi hiyo ni ile inayoshika kuanzia nafasi ya kwanza hadi ya 12.

“Ni kweli Tanzania watakuwa wakiingiza timu nne kwa kuwa klabu yake msimu huu imefanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa. “Pointi zimekuwa zikiongezeka kwa nchi kama klabu moja au mbili zimefanya vizuri, kwa hiyo sasa Tanzania watakuwa na timu mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na timu mbili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

“Kuhusu zitapatikana vipi hilo ni suala la Shirikisho la Soka hapa Tanzania kutengeneza mfumo lakini jambo pekee ambalo naweza kusema ni kwamba nawapongeza sana,” alisema Gaye raia wa Ivory Coast ambaye yupo hapa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana.

Hii ina maana kuwa kuna nafasi ya Simba, Yanga na timu nyingine ikiwemo Azam labda na Mtibwa Sugar kushiriki michuano ya kimataifa kwa msimu huo na kama zitakuwa zinaendelea kufanya vizuri basi zitakuwa zikifanya hivyo kila msimu.

Kwa mujibu wa msimamo wa Caf, Simba imepanda hadi nafasi ya 20 kwa ubora, ikiwa na pointi 15, lakini Tanzania yenyewe imepanda hadi nafasi ya 12 ikiwa na pointi 18, tatu ni zile ambazo ilizipata Yanga ilipotinga hatua ya makundi ya Kombe la Shrikisho msimu wa 2016/ 2017.

Nchi nyingine ambazo zina nafasi ya timu nne ni Morocco, Tunisia, Misri, Algeria, DR Congo, Afrika Kusini, Zambia, Sudan, Nigeria, Guinea, Angola na Tanzania.

2 COMMENTS:

  1. WAMESEMAJE??? WANASIKIA??? SHIDA TUPU.

    ReplyDelete
  2. Sasa hawa chura fc walivyokuwa wanawashabikia wageni hili hawakuwa wanalijuwa kweli hapo ndio tofauti mtu mwelewa na mbumbumbu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic