April 18, 2019


Kikubwa ambacho kinasumbua kwa sasa ndani ya ligi ni namna ya uendeshaji hasa kwa timu ambazo hazina udhamini kushindwa kumudu gharama zake na kusababisha wabuni njia isiyo rasmi ya kupitisha bakuli ili kumudu gharama.
Katika timu 20 ni chache sana ambazo zina uwezo wa kumudu gharama za uendeshaji wa timu zenyewe hali inayofanya michango kwa wanachama kuhusika kwa namna moja ama nyingine.
Kocha Msaidizi wa Lipuli, Seleman Matola ambaye ameshindwa kulinda rekodi yake kwa kutopoteza mchezo hata moja mbele ya mabosi wake wa zamani Simba baada ya kufanikiwa kutopoteza kwenye michezo mitatu ambayo amekutana nao ila wa nne mambo yakawa magumu tangu Lipuli ipande daraja, huyu hapa anafunguka mengi:-
"Kwa sasa kuna changamoto kubwa ambayo tunapitia hasa kwenye Ligi Kuu kutokana na kukosa kuwa na mdhamini mkuu ndani ya ligi hali ambayo inafanya usimamiaji kwa timu ambazo hazina wadhamini kuwa wa kusuasua.
"Tulianza kwa kuungaunga mzunguko wa kwanza sasa tupo mzunguko wa pili maumivu yanazidi kuwa makali kwa kuwa mpaka sasa hakuna dalili za milango kufunguka kwetu.
Tatizo kubwa limejificha wapi?

"Mfumo tulionao ndio unatuumiza, namaanisha kuanzia kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na wadau wengine ambao wanafikiria timu zinapata faida kubwa kumbe gharama za uendeshaji wa timu ndio kubwa.

Kwa nini TFF?

"Tulivyoanza Ligi hakuna ambaye alikuwa anajua kwamba hatutakuwa na mdhamini na hii yote inatokana na usiri uliopo, tunapata taarifa kwamba hatuna mdhamini mkuu wakati ligi inaanza sasa hakuna namna ni lazima timu ishiriki ili isikumbwe na adhabu.
Licha ya ugumu matokeo mazuri kwa timu yako yanabebwa na nini?
"Hakuna siri katika hili, tuseme ni baada ya mzunguko wa kwanza vijana kupata suluhu mbele ya Simba, kuliwaongezea kujiamini na kutambua kwamba wanaweza kufanya kitu kikubwa, hivyo kuanzia hapo tumekuwa na mwendelezo mzuri na bado tunapambana kupata matokeo.
Unadhani nini kifanyike ili kuboresha soka letu?
"Kuna mengi ya kuboresha hasa yatakayofanya kufanikiwa kupiga hatua kwa soka letu, kitu cha msingi ni kufanikiwa kuwekeza kwa vijana ambao wanachipukia, hawa watasaidia kupata wachezaji wazuri hivyo kama tutaanza kuwekeza kwa watoto kupitia kufungua vituo vya michezo.
"Mpira ni uwekezaji ili kufikia mafanikio katika hilo ni lazima tuanze kuwekeza kwa vijana ambao tunao na wakianza kupata mafunzo kutoka chini watafanya vizuri hapo baadaye.
Unaizungumziaje ligi ya Tanzania kwa sasa?

"Mengi yanatokea kwenye ligi yetu na ukweli ambao upo hayafurahishi bali yanaumiza hasa kwa baadhi ya timu kutokana na mtiriko wa matukio namna unavyokwenda ni pasua kichwa.
Kwa nini ukakasi?
"Hebu fikiria kuna timu ina mechi mkononi tano nyingine labda tuseme ni mbili au tatu sasa hapo lazima uwe ni ukakasi kwa sababu hakuna usawa ndani ya Ligi.
"Mechi tano mpaka nne ni nyingi sana ina maana katika hisia lazima utafikiria tu namna mazingira yanavyokuwa hasa kwenye soka letu la Tanzania.
Matokeo ya viporo ni nini?
"Kwa kadri viporo ambavyo vinakuwa kwa timu inaleta mazingira ya kubeba baadhi ya timu, kama TFF walikuwa wanatambua uwepo wa mashindano mengine yaliyopo basi ilipaswa mambo mawili yafanyike, kusimamisha ligi ama kutumia timu kikosi cha pili kuendelea kushiriki ligi ama Mapinduzi.
"Kwa sasa hali inavyokwenda inaweza kufika hatua timu ina viporo mpaka saba kutokana na aina ya mashindano na mvurugiko wa ratiba, muda wao utakapofika kucheza watakutana na timu ambazo hazina presha ya kupoteza chochote kwenye ligi hali itakayoleta hisia za kuwa na mazingira ya kubebana kwenye ligi.
Je kwa sasa uendeshaji wa timu ukoje?
"Timu nyingi zinaendeleza desturi ya kuomba, kwetu hali pia sio shwari kwani hakuna mdhamini ambaye msimu uliopita alikuwa anatupa sapoti kubwa hivyo nasi mzigo wetu wa uendeshaji unabebwa na viongozi pamoja na wadau ambao tunashirikiana nao.
"Lakini bado kuna ugumu wa uendeshaji hasa kutokana na hali ya uchumi kwa sasa kuwa sio nzuri, mashabiki na wadau waendelee kutupa sapoti ili tuendelee kufanya vizuri.
Hofu yako kubwa ni nini mzunguko wa pili?
"Kwa jinsi hali ilivyo ngumu kwa sasa upande wa uendeshaji wa timu kuna siku itatokea timu zitashindwa kusafiri kufuata mpinzani wake ama kama itafika itashindwa kurejea kama ambavyo mzunguko wa kwanza ilikuwa.
"Wachezaji wengi wanadai mishahara zaidi ya miezi mitatu ukichanganya na posho ni mzigo mkubwa sana ambao timu kwa sasa zinasimamia kuna haja ya kulitazama hili kwa ukaribu zaidi.
Je na kwa timu yako mambo yapoje?
"Hapa nazungumzia kiujumla namna hali ilivyo mzunguko wetu wa pili.
"Naogopa sana hali ilivyo, mkataba unazungumzia kuhusu mchezaji kuwa huru baada ya kutolipwa stahiki zake baada ya miezi mitatu hivyo kuna wachezaji ambao watashindwa kuendelea kutumikia timu zao endapo watatanguliza maslahi mbele.
"Kuna siku inaweza kutokea nikabaki uwanjani peke yangu kutokana na wachezji wengi kudai stahiki zao ila hilo sipendi litokee na ndio maana tunapambana kwa hali na mali kuweka usawa hasa katika kuwalipa stahiki zao.
Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo amesema kuwa mambo ambayo yanasababisha timu kuwa na viporo yapo wazi.
"Kila kitu kipo wazi hasa kwa timu ambazo zina viporo ligi kuu na mpangilio upo sawa kwa sasa kwa kuwa tayari ratiba za viporo zimepangwa ni jambo la wakati tu ili kuweza kuweka usawa katika haya," amesema.


1 COMMENTS:

  1. Ligi haitasimama hakuna tija kufanya hivyo kwa sasa. Timu zenye mvuto na kujituma uwanjani tutawachangia hata kwa kupitisha bakuli.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic