August 21, 2019


MICHUANO ya kimataifa kwa sasa imeanza kurindima hatua za awali kwa timu ambazo zimepata nafasi ya kushiriki michuano hiyo mikubwa huku Tanzania ikiwa na jumla ya timu sita kimataifa.

Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa kuna Simba, Yanga kwa upande wa Tanzania na KMKM kutoka visiwani Zanzibar na kwa upande wa Kombe la Shirikisho, Azam FC na KMC ni kwa upande wa Tanzania Bara huku Visiwani tukiwakilishwa na Malindi.

Mashabiki wameona namna timu zetu zote zilivyopambana kutafuta matokeo na mwisho wa siku baada ya dakika 90 za mwanzo kikapatikana kilichopatikana.

Nikukumbushe namna matokeo yalivyokuwa kwa timu ambazo zilikuwa ugenini, UD Songo 0-0 Simba, AS Kigali 0-0 KMC, Mogadishu City 0-0 Malindi, Fasil Kenema 1-0 Azam FC, zilizokuwa nyumbani ilikuwa hivi Yanga1-1 Township Rollers, KMKM 0-2 1st de Agosto.

Hapa tunaona kwamba ni timu moja tu ambayo imepoteza ugenini nayo ni Azam FC mchezo wa awali hayo ni matokeo ambayo yanaweza kubadilika kwenye mchezo wa marudio endapo wawakilishi wetu watachanga karata zao vema.

Simba, KMC  na Malindi ambao wamelazimisha sare ugenini wana kazi ngumu ya kufanya ili kupata matokeo nyumbani kwani kwa sasa kuna ile hali ya kuanza kupuuzia na kujipa ushindi kabla ya mchezo.

Kwenye ulimwengu wa mpira hakuna kitu hicho kazi bado ni nzito na wawakilishi wetu wakibweteka watafungwa nyumbani na kuwapa maumivu mashabiki na Taifa kiujumla.

Yanga ambao wamelazimisha sare nyumbani na KMKM ambao wamekubali kufungwa huu ni mpira na kila kitu kinawezekana wana nafasi ya kupata matokeo chanya ugenini.

Kikubwa ambacho kinapaswa kifanyike kwa sasa ni kwa timu zote kupanga mikakati mipya itakayowafanya waweze kupata matokeo chanya.

Mfano mzuri uwe kwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo inashiriki michuano ya Chan namna ilivyopenya hatua ya awali.

Wengi walikua wamekata tamaa juu ya Taifa Stars mwisho wa siku ikapenya tena ugenini hakuna ambaye aliamini.
Haya ndiyo maisha ya mpira hayahitaji kujiamini sana kitu cha msingi ni maandalizi na umakini ndio silaha kubwa ya ushindi kwenye michuano hii.

Kama ambavyo timu ya Wanawake ya Tanzania chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’ haikupewa nafasi kufanya vizuri ugenini mwisho wa siku wameshinda na kombe wametwaa licha ya kualikwa.

Hilo ni soma tosha kwa timu zetu kuacha kujiamini kupitiliza na badala yake ziwekeze nguvu kwenye maandalizi mazuri.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lisijisahau kwa sasa Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 24 baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii kuchezwa na Simba kuibuka kidedea mbele ya Azam FC.

Bado hakuna jitihada za wazi ambazo zinaonekana kuanza kwa mdhamini pamoja na mpango wa kubadilisha ratiba iendane na michuano ya kimataifa.

Ukimya huu unalea shaka kwamba huenda msimu ujao tutakuwa na mzigo mkubwa wa viporo kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Maandalizi ni muhimu kwa ligi ikiwa na ushindani itasaidia kupata wachezaji bora na makini kwa ajili ya Taifa letu ambao ni hazina kwenye timu ya Taifa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic