August 21, 2019


TANZANITE, timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 20 imefanya makubwa kwenye ulimwengu wa soka la wanawake na dunia kwa sasa inatambua.

Vijana walialikwa kwenye michuano ya COSAFA ambayo imemalizika nchini Afrika Kusini na wamepambana mpaka wametwaa kombe la COSAFA ni mafanikio makubwa.

Kwa walichofanya wanastahili pongezi kwani wameonyesha kwamba Tanzania kuna vipaji ambavyo vikipewa nafasi ya kufanya vizuri vinaleta matokeo chanya.

Mwendelezo uwe kila siku kwa timu zote na uwekezaji ukiwa mkubwa utasaidia kuleta ushindani mkubwa wakati mwingine.

Hongera kwa benchi la ufundi wachezaji pamoja na wadau ambao wamekuwa bega kwa bega kuipa sapoti timu ya Tanzanite.

Mafanikio hayo yawape hasira wachezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana, chini ya miaka 15 ambao wanashiriki michuano ya CECAFA nchini Eritrea kufanya kweli.

Tumeona wameanza kwa kuchechemea mchezo wa kwanza dhidi ya Uganda kwa kufungwa mabao 2-0 na leo wana kazi nyingine mbele ya Sudan wanapaswa wapambane.

 Mambo yamezidi kunoga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sasa ambapo kila timu ipo bize kusaka matokeo uwanjani hasa ukizingatia kwamba raha ya mchezo ni matokeo chanya.

Tumeona namna hali ilivyokuwa kwa wawakilishi wetu wa Tanzania namna ambavyo wameanza kwa juhudi na kuonyesha kwamba walijipanga kushiriki michuano hii mikubwa ndani ya Bara letu la Afrika.

Azam FC wawakilishi wa Kombe la Shirikisho Afrika wao wameanza ugenini na kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Fasil Kenema ya Ethiopia.

Licha ya kupoeza mchezo wa awali bado kuna nafasi kwa Azam FC ambao wanapeperusha Bendera ya Tanzania kupata ushindi kwenye mchezo wa marudio.

Wapinzani wao wametumia vizuri uwanja wa nyumbani nao wana kazi ya kutumia vema uwanja wa nyumbani kwenye mchezo wa marudio ili kupaa matokeo chanya.

Yanga wao walianza nyumbani na kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wapinzani wao Towsnship Rollers kutoka Botswana kete moja wanayo mkononi ni ya ushindi.

Kama waliweza kupata angalau bao moja nyumbani basi hata ugenini wana nafasi ya kushinda na kusonga mbele endapo watajipanga na kujiaandaa vizuri.

 Kikubwa ambacho wanatakiwa kukifanya ni kuongeza maarifa zaidi kwenye mchezo wa marudio ili wawe makini zaidi ya ule wa awali ambao walikuwa na nafasi ya kushinda mapema nyumbani.

Makosa yao yaliyopita yanapaswa yafanyiwe kazi ili wawafuate wapinzani wao wakiwa wamekwiva na nia yao iwe moja kupata ushindi kwenye mchezo wa marudio na hatimaye kusonga mbele kwenye michuano hii mikabwa.

Mchezo wa nyumbani mara nyingi tathimini ya wengi huegemea kwenye ushindi ukizingatia kwamba kuna nguvu ya mashabiki ila kwenye mpira matokeo huzungumzwa baada ya dakika 90.

Kwa makosa ambayo yapo yafanywe kazi ili kupata ushindi na kazi hiyo inapaswa ianze kwenye benchi la ufundi wachezaji pamoja na mashabiki kuwapa sapoti wachezaji kwenye mchezo wa marudio.

KMC ambao ni wawakilishi kwa upande wa Tanzania Kombe la Shirikisho, Simba wawakilishi wa Tanzania kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Malindi wawakilishi wa Zanzibar michuano ya Kombe la Shirikisho hawa walilazimisha sare ya bila kufungana ugenini.

Kazi yao sasa sio ndogo kwenye mechi za marudio wanapaswa watambue kwamba watakuwa nyumbani na kazi yao itakuwa ni kutafuta matokeo chanya.

Hivyo wanapaswa watumie mtindo wa kushambulia mwanzo mwisho ili kupata mabao mengi ya mapema kisha wavute pumzi kushusha presha.

Endapo wataruhusu kufungwa mapema kazi yao itaongezeka ugumu na mwisho wa siku wanaweza kutolewa tena wakiwa nyumbani jambo ambalo watanzania hawatakwa na furaha kuona likitokea.

Wachezaji pamoja na benchi la ufundi linapaswa lifanyie kazi makosa ya uzembe wa kutumia nafasi ambazo wanazipata pamoja na mabeki kuongeza ulinzi kwenye safu yao ya ulinzi ili kutoruhusu nyavu zao kuonewa mapema.

Hakuna kujilinda kwenye mchezo wao wakiwa nyumbani ni kutafuta ushindi huku mashabiki wakishangilia mwanzo mwisho kwenye michezo ya marudio.

Ngoma bado inaruhusu kwa KMMK ya Zanzibar ambao wanaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa kwenda kupindua meza mbele ya wapinzai wao wa Angola kama wao wamewafunga mabao 2-0 nyumbani bas nao wana nafasi ya kushinda kwa mabao zaidi ya mawili.

Wachezaji wajiamini na wacheze kwa juhudi kubwa kutafuta matokeo kufanikiwa kwa timu zetu zote sita kimataifa ni hatua kubwa na itakuwa furaha kwa mashabiki na faida kwa wachezaji wetu kujiweka kwenye ramani ya soko la biashara.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic