CHIRWA: NITAANZA NA YANGA KWANZA
Staa mpya wa Azam FC, Obrey Chirwa amefunguka kwamba moja ya malengo yake kwa sasa ni kuwafunga mabosi wake wa zamani Yanga na kuipa ubingwa klabu yake ya Azam FC baada ya kujiunga nao.
Chirwa, jana Alhamisi alitambulishwa rasmi kuwa mchezaji mpya wa Azam FC ukiwa ndiyo usajili wa kwanza wa klabu hiyo kuelekea kipindi cha dirisha dogo la usajili.
Mshambuliaji huyo raia wa Zambia ametua Azam FC inayofundishwa na Kocha Hans van Pluijm akiwa mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba na Klabu ya Nogotoom ya Misri ambayo alikuwa anaichezea.
Chirwa amesema kwamba kwake jambo ambalo liko mbele kwa sasa ni kuhakikisha kwamba klabu yake hiyo inatwaa ubingwa wa ligi lakini sambamba na kuzifunga Yanga na Simba pale atakapokutana nazo.
“Ninashukuru kujiunga na Azam FC ninaomba mashabiki wanipokee vizuri, nitahakikisha ninafunga mabao kumi, pamoja na kuzifunga Yanga na Simba kwa sababu hizo ndizo ambazo zinakufanya mtu jina liwe juu.
“Nilishindwa kutua Yanga kwa sababu kocha wao, Mwinyi Zahera alinikataa nisijiunge,” alisema Chirwa.
Akimzungumzia Chirwa, Kocha Pluijm alisema: “Ninamjua vizuri Chirwa ni mtu ambaye nimefanya naye kazi vizuri sana. Ana kasi na hakati tamaa kwa kitu ambacho anakipambania, nina imani atatusaidia sana kwenye safu yetu ya ushambuliaji,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment