Polisi Morogoro inapambana na Ruvu
Shooting katika moja kati ya mechi tatu za Ligi Kuu Bara
zitakazochezwa kesho (Aprili 10 mwaka huu). Matokeo ya mechi hiyo yanatarajia
kutoa mwanga kama Polisi inaweza kubaki kwenye ligi hiyo msimu ujao.
Timu hiyo itakuwa nyumbani Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro katika mechi hiyo itakayochezeshwa na Ibrahim Kidiwa
kutoka Tanga akisaidiwa na Godfrey Kihwili na Ephrony Ndissa wa Arusha.
Polisi Morogoro inayonolewa na Adolf
Rishard inakamata nafasi ya mwisho ikiwa na pointi 18 tu na imebakiza mechi
tatu dhidi ya Simba, Kagera Sugar na Coastal Union.
Mechi nyingine za kesho ni kati ya
Tanzania Prisons iliyo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 20 dhidi ya Mgambo
Shooting. Mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi
hiyo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya. Mgambo ina pointi 24
na iko katika nafasi ya tisa.
Mwamuzi Said Ndege wa Dar es Salaam
atachezesha mechi kati ya wenyeji Mtibwa Sugar na Toto Africans itakayofanyika
Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Toto Africans ya Kocha John
Tegete ina pointi 21 ikiwa nafasi ya 11 wakati Mtibwa Sugar iko nafasi ya tano
na pointi zake 32.
Ligi hiyo itaendelea keshokutwa
(Aprili 11 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Azam na African Lyon itakayofanyika
Uwanja wa Azam Complex.
0 COMMENTS:
Post a Comment