KLABU ya Yanga na Kocha Msaidizi wa
timu ya Toto Africans, Athuman Bilali wamepigwa faini ya sh. 500,000 kila mmoja
kutokana na makosa mbalimbali katika mechi za Ligi Kuu ya Bara inayoendelea nchini.
Adhabu hizo zimetolewa na Kamati ya
Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Jumapili
(Aprili 7 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia ripoti za waamuzi na
makamishna kwa michezo namba 108 hadi 171.
Yanga imepigwa faini hiyo baada ya
kupata kadi tano za njano katika mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa
Februari 7 mwaka huu. Vilevile Kagera Sugar imepigwa faini ya sh. 100,000 kwa
kuchelewa kufika kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) dhidi
ya African Lyon iliyochezwa mjini Bukoba, Februari 23 mwaka huu.
Naye Kocha Bilali amepigwa faini
hiyo na kufungiwa mechi tatu za ligi hiyo kwa kumshambulia kwa maneno kocha wa
timu pinzani, hali iliyosababisha mwamuzi amtoe kwenye benchi la wachezaji.
Alifanya tukio hilo kwenye mechi kati ya Toto Africans na Tanzania Prisons
iliyochezwa Aprili 3 mwaka huu jijini Mwanza.
African Lyon na Simba zimepigwa
faini ya sh. 500,000 kila moja kwa kushindwa kuchezesha timu zao za U20 kwenye
mechi za utangulizi wakati zilipocheza na Oljoro JKT na Coastal Union, Machi
mwaka huu kwenye viwanja vya Azam Complex na Uwanja wa Taifa.
Suala la Meneja wa Coastal Union,
Akida Manchai kumshambulia kwa maneno yasiyo ya kiungwana Makamu Mwenyekiti
wake Steven Mnguto baada ya kwenye mechi kati ya African Lyon na Coastal Union
iliyochezwa Machi 30 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex limepelekwa Kamati ya
Nidhamu kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa
Kanuni za Ligi Kuu Kuu Bara.
BONIFACE
WAMBURA
MSEMAJI
TFF
0 COMMENTS:
Post a Comment