Baada ya Yanga kufanya mazoezi ya kusuasua kwa
muda wa wiki mbili, sasa mambo yamekaa sawa baada ya kikosi cha timu hiyo kuwa
sawa kufuatia nyota wake wa kimataifa kutua nchini.
Tangu kikosi cha Yanga kianze mazoezi yake ya
kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, kilikuwa kikiundwa na wachezaji
wachache, jambo ambalo lilikuwa likimpatia wakati mgumu kocha mkuu wa timu hiyo
raia wa Uholanzi, Hans van Der Pluijm kuanza mikakati yake.
Hata hivyo, baada ya nyota hao wa kimataifa wa
timu hiyo ambao ni Mrundi, Amissi Tambwe na Wanyarwanda Haruna Niyonzima pamoja
na Mbuyu Twite kutua nchini, sasa kikosi cha timu hiyo kipo kamili gado tayari
kwa kuanza rasmi maandalizi yake kwa ajili michuano hiyo.
Kwa pamoja wachezaji hao na wale waliokuwa na
kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ wataungana na wenzao leo hii katika
mazoezi yatakayofanyika kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
Pluijm alisema ujio wa nyota hao, utamwezesha
kuanza rasmi mikakati yake kwa kasi ya ajabu.
“Mazoezi yetu ya awali yalikuwa siyo mabaya
sana ila kuanzia kesho (leo) mambo yatakuwa mazuri zaidi kwani nitakuwa na
sehemu kubwa ya wachezaji wangu na hapo ndipo nitakapoanza kuitekeleza rasmi
mikakati yangu kwa ajili ya msimu ujao.
“Tambwe na Twite tayari wameshatua nchini
lakini pia wale waliokuwa na Taifa Stars nao tunaweza kuwa nao katika mazoezi
yetu ya kesho (leo),” alisema Pluijm.
Katika hatua nyingine, Pluijm ameeleza kufurahishwa
na uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuruhusu klabu za ligi kuu
kusajili wachezaji saba wa kigeni kutoka watano kama ilivyokuwa hapo awali.
“Nimefurahishwa
sana na hatua hiyo ya TFF, hivyo ni matumaini yetu kuwa utasaidia kwa kiwango
kikubwa klabu za Tanzania kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na sasa
tunajipanga kuongeza nyota wengine ili kukiimarisha kikosi chetu,” alisema.
Kwa sasa Yanga ina wachezaji watano wa
kimataifa ambao ni Tambwe, Twite, Niyonzima, Kpah Sherman na Andrey Coutinho.
0 COMMENTS:
Post a Comment