Yaleyale! Jinamizi la timu ya Kagera Sugar kukimbia makazi limeendelea
kuwatesa, baada ya kutangaza kuachana na Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, ambao
wamekuwa wakiutumia kama uwanja wao wa nyumbani.
Timu hiyo ambayo inakodi uwanja kutokana na wao wa Kaitaba kuwa
kwenye ukarabati wa kisasa, imesema kwa sasa mikakati iliyopo ni kutaka kusogea
karibu na Ukanda wa Pwani ambako ndiko kuna timu nyingi za ligi kuu.
Ikumbukwe kuwa msimu uliopita Kagera walitumia viwanja viwili
tofauti; CCM Kirumba wa Mwanza, kabla ya kuhamishia makazi Kambarage, Shinyanga,
kwa kile kilichosemwa kuwa Kirumba walikuwa wakifanyiwa hujuma za kishirikina
kutoka kwa wanachama waliodhaniwa kuwa wa Toto Africans.
Mratibu wa timu hiyo, Mohamed Hussein ameliambia Championi
Jumatano kuwa; “Tunataka kusogea karibu na Ukanda wa Pwani maana timu nyingi
ziko huko. Lakini pia hata ratiba ya ligi kuu inatubana sana, tofauti na misimu
iliyopita mechi zilikuwa wikiendi tu.
“Lakini msimu huu tunacheza mara mbili kwa wiki na huku ni mbali
sana- wachezaji hawapati muda wa kupumzika, hivyo tumeona tusogee karibu na sehemu
yenye timu nyingi,” alisema.
Hata hivyo, imeaminika kuwa matokeo mabovu kwenye uwanja huo pia
yamechangia Wakata Miwa hao kukimbia.
0 COMMENTS:
Post a Comment