July 9, 2017


Kaimu Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amewapa kongole viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake (TWFA), waliochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Chichi, Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo uliopata uwakilishi wa theluthi mbili ya mikoa yote ya Tanzania, Amina Karuma alitetea kiti chake kwa kupata kura 47 kati ya 52 za wapigakura wote huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti ikichukuliwa na Rose Kissiwa ambaye aliyepata kura 42.

Mwanahabari Mkongwe wa Gazeti la Nipashe kutoka Jumba la Magazeti la The Guardian, Somoe Ng’itu alishinda nafasi ya Katibu Mkuu kwa kuvuna kura 49 ilihali Theresia Mung’ong’o alishinda nafasi ya Katibu Msaidizi.

Hilda Masanche alishinda nafasi ya Mweka Hazina wa TWFA kwa kupata kura 25 wakati Mwanahabari mwingine Zenna Chande alishinda nafasi ya Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kupata kura 44.

Wajumbe Triphonia Temba, Mwamvita Kiyogoma, Jasmine Soudy na Chichi Mwidege hawakushinda baada ya wagombea wote wanne kutopata zaidi ya nusu ya kura kulingana na idadi ya wapigakura kwa mujibu wa katiba ya TWFA.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Msomi Wakili George Mushumba, ambaye pia aliwapongeza washindi.

Awali akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi aliwataka wajumbe hao kuwa makini katika kuchagua na kwamba si wakati wa kufanya mzaha katika soka la wanawake.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV