YANGA YAPATWA JEURI NA STRAIKA HUYU, WALETENI TU SIMBA
Baada ya Simba kushinda jioni, Yanga ilijibu mapigo kwa kushinda usiku huku Amissi Tambwe akirejea kwenye makali yake kwa kufunga mabao mawili ‘brace’.
Timu hizo zimeshinda kuelekea kwenye mchezo wao utakaochezwa Septemba 30, na sasa kila upande baada ya ushindi huo ni kama wanasema: “Waleteni sasa” kutokana na kujiamini kwamba unaweza kuibuka na ushindi.
Yanga juzi iliichapa Singida United mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, huku Ibrahim Ajibu akipiga pasi ya bao la kwanza la Tambwe na kufikisha jumla ya asisti tano katika mechi nne ambazo Yanga imecheza kwenye Ligi Kuu Bara.
Ajibu alitoa asisti (pasi za mabao) tatu katika mechi dhidi ya Stand, akatoa asisti nyingine dhidi ya Coastal, kabla ya jana kutoa nyingine.
Ushindi huu unaashiria sasa Yanga ipo tayari kukutana na Simba Jumapili ijayo, ikiwa imeshinda mechi zote nne ilizocheza kwenye Ligi Kuu Bara na kupanda kileleni mwa msimamo.
Tambwe ambaye wengi walianza kumuona amechuja na ‘ameshazeeka’, alianza kufunga dakika ya 29 kwa kichwa akiunganisha krosi ya Ajibu, aliongeza bao la pili dakika ya 45+2 kwa pasi fupi ya Gadiel Michael na kuamsha shangwe la mashabiki wa timu yake.
Kocha Mwinyi Zahera alifanya maamuzi magumu kwa kuamua kutowatumia beki Kelvin Yondani na washambuliaji wake hatari Heritier Makambo na Mrisho Ngassa, na akawashangaza wengi alipoamua kuwaanzisha Tambwe na Matheo Anthony.
Aliamua kuwapumzisha nyota hao kwa kile kilichoonekana ni mchezo dhidi ya watani Jumapili hii.
Yanga: Benno Kakolanya, Paul Godfrey, Gadiel Michael, Abdallah Shaibu, Andrew Vincent ‘Dante’, Feisal Abdallah, Deus Kaseke, Papy Tshishimbi, Tambwe, Ajibu na Anthony.
Singida: David Kissu, Kennedy Juma, Mohammed Tello, Elisha Muroiwa, Rajab Zahir, Yusuph Kagoma, Athanas Mdamu, Amara Diaby, Hans Kwofie, Kenny Ally na Geofrey Mwashiuya.








0 COMMENTS:
Post a Comment