WAWILI YANGA WAIVURUGA SIMBA
Wakati homa ya mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga ikizidi kupamba moto, washambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo na Ibrahimu Ajibu wamezua balaa ndani ya kikosi cha Simba.
Wachezaji hao kwa sasa ndiyo wanaozungumzwa sana ndani ya kikosi cha Simba kabla ya timu hizo kukutana uwanjani Septemba 30.
Mpaka kufikia juzi jioni, kabla ya Yanga kupambana na Singida United, wachezaji hao walikuwa wameitumikia timu hiyo mechi tatu huku Makambo akiongoza kwa kuzifumania nyavu ndani ya kikosi hicho akiwa amefunga mabao mawili, wakati Ajibu akiongoza kwa kutengeneza nafasi za kufunga kuliko wachezaji wengine wote wa ligi kuu, alikuwa ametengeneza nafasi nne na kufunga bao mmoja.
Hata hivyo, baadhi ya wachezaji wa Simba wanaodaiwa kuwazungumzia zaidi wachezaji hao ni kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude.
Alipoulizwa kuhusiana na hilo, Mkude aliliambia Championi Jumatatu kuwa ni kweli wamekuwa wakiwajadili wachezaji hao, na hiyo ni kutokana na uwezo ambao wamekuwa wakiuonyesha katika mechi zilizopita.
“Hakuna asiyeujua uwezo wa Ajibu anapokuwa uwanjani, binafsi naheshimu sana uwezo wake, kama umesikia kuwa tunamzungumzia, basi ni kwa sababu hiyo.
“Hata hivyo, naamini kuwa tutakabiliana naye pamoja na wachezaji wengine wote tutakaokutana nao uwanjani katika mechi hiyo endapo Mungu atatufikisha salama,” alisema Mkude.








0 COMMENTS:
Post a Comment