Yanga ina majina mawili ya Makocha mezani ambayo mmoja wao ndiye atakayekuwa kocha msaidizi wa Yanga kuanzia mwezi ujao na wote ni vijana machachari.
Ingawa bado mchakato wa kocha mkuu unaenda taratibu lakini Yanga wako kwenye mjadala mzito wa yupi wampitishe kama msaidizi kati ya Kally Ongala na Mecky Maxime ambaye kwa sasa yuko na Kagera Sugar.
Ongala ambaye ni raia wa Uingereza aliyekulia Sinza, amewahi kuichezea na kuifundisha Azam kwa vipindi tofauti huku Yanga wakiamini kwamba ana mapenzi makubwa na timu yao.
Imefahamika kuwa, hatma ya kocha msaidizi itajulikana wikiendi hii itakapokutana Kamati ya Ufundi chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Charles Mkwasa.
Lakini Yanga wamepanga kumpa Mkwasa nafasi ya kukaimu mpaka baadaye mwakani watakapoleta kocha mkuu lakini mchakato wa kina Ongala na Maxime unatakiwa kumalizika mapema.
Alipotafutwa Maxime kuzungumzia hilo alisema kuwa “Nipo tayari kutua Yanga muda wowote hata hivi sasa, kikubwa ni tukubaliane maslahi tu ya kazi yatakayonishawishi mimi kufanya kazi nao.
“Kwa sasa nipo Morogoro nimepumzika, hivyo kama wananitaka, ni tayari hata leo wao wanitumie nauli, haraka nitakuja huko Dar kwa ajili ya kumalizana nao,” alisema Maxime ambaye alistaafu Taifa Stars kwa heshima.








0 COMMENTS:
Post a Comment