Na Saleh Ally
KIUNGO mkongwe
nchini Amri Kiemba yuko kwenye mgogoro na uongozi wa klabu yake kwa madai
kadhaa ambayo yanaunganishwa na utovu wa nidhamu.
Kiemba
anatuhuma nyingi za chinichini, lakini kati ya hizo, lililozungumzwa ni
kuhusiana na kuonyesha kiwango cha chini katika mechi anazoichezea Simba.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope yeye alisema hadharani kabisa
kuonyesha hafurahishwi na jambo hilo.
Pia akasisitiza
kwamba, alipoingia Kiemba katika mechi dhidi ya Prisons, wenyeji wakasawazisha
kwa kuwa yeye alifanya uzembe. Hata hivyo, Hans Poppe, alisisitiza alihadithiwa
ilivyotokea.
Siku moja
baadaye uongozi wa Simba kupitia Kamati ya Utendaji ulitangaza kuwasimamisha
Shabani Kisiga, Haroun Chanongo na Amri Kiemba.
Leo ndiyo
itakuwa siku ya hukumu watakapokaa na uongozi na kila mmoja kuzungumza
alichonacho kabla ya kuangalia kipi sawa na kipi si sahihi.
Kabla hata
hawajakaa, Kiemba tayari amehojiwa na vyombo vya habari na kuweka wazi kwamba kama
riziki yake na Simba itakuwa imefikia mwisho, basi hana lolote la kupinga. Kwa
maneno hayo, ni sahihi kusema Kiemba yuko tayari kwa lolote.
Taarifa kutoka
ndani ya Simba zilieleza kwamba tayari Kiemba alihojiwa na baadhi ya viongozi
wa Simba, kwamba kwa nini amekuwa akicheza chini ya kiwango akiwa na Simba,
halafu anafanya vizuri akiwa na Taifa Stars.
Yeye akawajibu
kwamba, akiwa Taifa Stars hana presha na anacheza kwa kufuata maelekezo ya
mwalimu na si kufuata anachotaka mwalimu na wengine.
Inawezekana ni
fumbo, wanachotaka wengine ni kina nani, viongozi wa Simba au kina nani? Rafiki
zake Kiemba au vinginevyo lakini inaonyesha viongozi watakuwa wamemuelewa ana
maanisha nini!
Neno lake kama
riziki imeisha pia lina tafsiri kubwa sana, kwamba Kiemba anaona anaweza
kuondoka. Hilo si tatizo, lakini kuna kila sababu ya viongozi kabla ya kukaa na
Kiemba, basi watafakari.
Kwamba kabla ya
kuitwa Taifa Stars, alikuwa akifanya vizuri Simba, ndiyo maana akateuliwa
katika kikosi hicho cha taifa. Asingeweza kuteuliwa kama angekuwa anaboronga.
Chanzo cha
Kiemba kushuka ni kipi, uwezo umepungua, ana matatizo nje ya mpira, kuna kitu
hakimridhishi ndani ya Simba?
Pia wanaweza
kutafakari mambo mawili, kwanza ni namba anayochezeshwa Simba na ile ya
Taifa Stars
ziko sawa?
Pili Simba
wajiulize, mfumo wa Makocha Patrick Phiri na ule wa Mart Nooij wa Taifa Stars
unafanana au unaweza kuwa sawa kwa Kiemba?
Ninamjua Kiemba
kuwa ni mmoja wa watu wasiohofia kusema ukweli bila ya kujali yuko wapi na
wakati gani.
Ninavyoona,
kama Kiemba angekuwa hafai kwenye mfumo wa Phiri, basi asingekuwa anamtumia
kwenye kikosi chake iwe kwa kuanza au kumuingiza kipindi cha pili.
Tukubaliane,
kutokana na uzoefu wake mkubwa katika soka, Phiri anajua zaidi kuliko Hans Pope
au viongozi wengine wa Simba kuhusiana na Kiemba anafaa au la.
Kuna jambo
jingine la kulifanyia kazi pia, kuwa kama Kiemba alicheza soka safi wakati wa
Milovan Cirkovic na Zdravko Logarusic, vipi sasa wakati wa Phiri au naye kuna
kitu anachompa kinamshinda?
Ndiyo maana
Simba wanapaswa kuwa na umakini mkubwa, wafanye uchunguzi wa kutosha kabla ya
kuanza kikao cha leo.
Wakati
wanashughulikia suala lake pia wenzake, yaani Kisiga na Chanongo wanapaswa
kuangalia suala la ukweli na haki. Kwamba kama mchezaji atasema ukweli na
wakaona kuna jambo la kulishughulikia, basi wasichukulie jazba au kwenda kwenye
kikao wakiwa na maamuzi yao tayari.
Viongozi Simba wasitafute kujikosha, tatizo ni usajili wa mbwembwe usiozingatia mahitaji ya timu! Okwi sawa, lakini kwanini wasingeangalia mtu wa kumkata kwa nafasi inayolingana au karibu na ya Okwi matokeo yake wanabomoa beki ambayo ni tatizo toka msimu uliopita na ilianza kutulia! Bora wangemuacha Kwizera au Kiongera kuliko Musoti! Watawatuhumu wachezaji wakati beki haijatulia! Huo ni ufinyu wao wa kufikiri kiufundi na kufikiri kishabiki!
ReplyDelete