Uongozi wa Kagera Sugar umeamua kuhamia mkoani
Shinyanga na kuachana na Uwanja wa CCM Kirumba kwa kile kilichotajwa kurogwa na
wenyeji wa uwanja huo, Toto African, kwa sababu zilizotajwa kuwa waliapa
kuhakikisha Kagera haitoki na pointi uwanjani hapo.
Chanzo cha bifu lao ni kwamba Toto wanalipiza
kisasi cha Kagera kuwabania misimu miwili iliyopita ambapo iliwafunga katika
mchezo wa mwisho, kichapo kilichowashusha daraja Toto African licha ya Kagera
tayari ilikuwa imejihakikishia pointi za kubaki ligi kuu.
Kagera Sugar ilihamishia maskani yake kwenye
Uwanja wa Kirumba, kutokana na uwanja wao wa nyumbani, Kaitaba, kuwa katika
matengenezo lakini vichapo vitatu mfululizo kutoka kwa Azam, Mbeya City na cha
juzi dhidi ya Ndanda vimewatia shaka.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya Kagera,
kimesema kuwa wamekubaliana kuhamia mkoani Shinyanga
ambapo mechi zao zote watachezea mkoani humo.
“Waswahili
wanasema lisemwalo lipo, sawa, hakuna mwenye uhakika na kinachosemwa, lakini
kadiri mechi zinavyokwenda, tunazidi kuingiwa na hofu. Tulianza kusikia watu wa
Toto wakisema hivyo katika mechi ya kwanza na Mbeya, maneno hayo yakaendelea
kwenye mechi zilizofuatia, lakini sasa tumeanza kuamini. Kila mmoja anaujua
uwezo wa Kagera, kabla ya kuja Mwanza ilikuwa imepoteza mechi moja tu kati ya
nane.
“Hivi kweli sisi ndiyo wa kufungwa mechi tatu
mfululizo? Haijawahi kutokea timu hii ifungwe namna hii, tumeanza kuamini imani
za kishirikina kama siyo mbinu chafu za wenyeji wetu wanazotuambia hadharani,”
alisema mtoa habari.
Alipotafutwa Mratibu wa Kagera, Mohammed
Hussein, alikiri kusikia maneno hayo na kuongeza kuwa tayari wamehamishia
makazi yao mkoani Shinyanga.
“Ni kweli nimeyasikia maneno hayo si mara moja
na tumeamua kuhamia mkoani Shinyanga ambapo mechi zote tutakuwa tukichezea huko,” alisema Hussein.
0 COMMENTS:
Post a Comment