September 15, 2018





NA SALEH ALLY
NIMEONA niendelee na Simba kwa kuwa tayari wametangaza njia yao kwenda katika mabadiliko. Kutoka klabu inayoendeshwa kimazoea hadi kuwa klabu inayoendeshwa kitaalamu.

Utaalamu ni nini? Hakuna ubishi lazima wawepo watu waliosomea masuala fulani ambayo yanahusiana na uendeshaji wa Klabu ya Simba.

Bila ubishi hata kama itakuwa na uongozi, Simba itahitaji kitengo bora cha masoko, makocha sahihi, timu ya watafuta vipaji na kadhalika.

Simba lazima iende katika njia mbili. Kwanza ni uwanjani ambako itakuwa na wataalamu wa masuala ya uwanjani ambao watatakiwa kupewa nafasi yao ili waweze kufanya kazi kwa ufasaha na kadhalika.

Lakini wataalamu ambao watakaa ofisini na kazi yao inakuwa ni kupanga na kuendeleza mipango sahihi wakiitumia timu yao ili kupeleka maendeleo katika Klabu ya Simba.

Tunaweza kuyapitia yote hayo kadiri tunavyosonga mbele lakini kuna mambo muhimu ambayo Simba lazima wayafanye ili kuonyesha kwamba wamekwenda katika mabadiliko na klabu yao sasa imeweza kumilikiwa na mtu mmoja binafsi (baada ya kuwa wamefikia hili) pamoja na wanachama wengine.

Maana kama watafikia, mwekezaji atakayepewa nafasi, atapewa hisa ya asilimia 49, anaweza kuwa Mohamed Dewji au mtu mwingine. Pia anaweza kuwa mtu mwingine pia ambaye ana nia ya kuendeleza lakini wanachama watabaki na asilimia 51 ya umiliki. Pamoja na yote hayo, haya yafuatayo hayatakwepeka ili kukimbilia maendeleo.

 Wataalamu:
Wataalamu ndiyo wale nilioanza kuwagusa. Kawaida klabu kama Simba pamoja na ukubwa wake zimekuwa zikiendeshwa kienyeji sana. Viongozi wake wamekuwa wale watu wanaoamini wanajua kumbe sivyo.
Simba yenye mabadiliko lazima iwe na vitengo kadhaa na muhimu sana suala la wataalamu wa masoko ambao wataipangia Simba njia sahihi ya kupita kwenda katika maendeleo.

Wataalamu wa masoko wataangalia bidhaa za Simba zina thamani ipi, watafanya mipango sahihi ya kupita kuzipandisha na wao ndiyo watahusika na namna ambavyo Simba inaweza kuingiza fedha kwa kuwa Simba sasa ni kampuni ya kibiashara.
Wataalamu hao wa biashara wanapaswa kuwa ni wale walio katika biashara ya soka, wanajua nini cha kufanya au wanatokea katika tasnia ya wataalamu wa biashara lakini ni Watanzania wanaojua thamani ya Simba na namna gani waitengeneze.
Lazima wataalamu hawa wapewe nafasi ya kufanya kazi yao. Lakini lazima wabanwe kuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu kuhakikisha Simba inafika ambako wamepanga.


Uwanja wa mazoezi:
Simba ni klabu na inamiliki timu, inatakiwa kuwa na kikosi imara ambacho kitalifanya soko lake kupanda. Hauwezi kuwa na timu inayofungwa kila mara halafu soko lako likawa kubwa. Mafanikio makubwa uwanjani ni sehemu ya uboreshaji wa soko la klabu husika.
Hivyo, ili kuwa na timu imara, Simba lazima iwe na timu imara inayofanya vizuri Tanzania, ukanda wa Afrika Mashariki na ikiwezekana Afrika kote. Hii italifanya soko lake kukua na kupanda maradufu.
Uwanja wa uhakika wa mazoezi utaifanya Simba kuwa imara. Utaifanya kuwa na maandalizi sahihi kwa timu kuanzia ya wakubwa na zile za vijana na watoto au wanawake pia.

Simba ikiendelea kuwa na viwanja vya kukodi, pia inapunguza heshima na inapunguza mwonekano wa watu makini kwa kuwa wana timu inayoshiriki hadi michuano mikubwa ya Afrika, lakini hawana uwanja wa mazoezi!

Hoteli/hosteli:
Kati ya vitu vinavyochota fedha nyingi katika timu ni kambi. Kunapokuwa na maandalizi hasa kwa nchi za Afrika kunatakiwa na mkusanyiko wa pamoja wa wachezaji ambao huitwa kambi.
Ulaya, mfano Real Madrid wana hoteli ya nyota tatu ndani ya viwanja vyao vya mazoezi. Kuna eneo kubwa lijulikanalo kama Ciudad Madrid, nje kidogo ya Jiji la Madrid.


Eneo hilo lina viwanja 13 vya mazoezi, sehemu ya gym, uwanja wa ndani wa mazoezi na kadhalika. Lakini kuna hoteli hiyo ambayo inawapunguzia wao kuingia gharama za muda mrefu wanapohitaji wachezaji wao kukaa pamoja.
Simba wanapaswa kuwa na eneo la namna hiyo kwa kuwa sasa wanatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kambi wakati timu inaingiza fedha kiduchu kabisa. Maisha ya Simba yamekuwa ni kutumia nyingi na kuingiza kidogo, maisha haya hata kama ni yale ya kawaida, anaweza kuishi mwendawazimu pekee. Huu ndio wakati wa kubadilika.
Kwenye Uwanja wa Bunju unaomilikiwa na Simba, wanaweza kuwa na viwanja viwili na sehemu angalau kwa ajili ya hoteli ya nyota tatu ambayo kama timu yao haipo kambini au hawaitumii, wanaweza kuitumia kama sehemu ya biashara kwa kuzikodisha klabu nyingine zikawa zinalipa, nayo ikawa ni sehemu ya kupunguza gharama lakini pia ya kuongeza kipato.

Kikosi cha watoto:
Miaka mingi Simba imekuwa na kikosi cha watoto. Lakini kinakwenda kwa mwendo wa kubahatisha, hiki ni lazima kiandaliwe kwa usahihi mkubwa.
Kuwa na kikosi bora cha watoto ni kutengeneza msingi wa ubora wa kikosi lakini pia kujenga biashara bora ya baadaye kwa kuwa wachezaji pia wanauzwa.

Biashara:
Kuuza wachezaji ni biashara na si mapenzi au matakwa ya moyo. Hivyo inawezekana Simba ina mchezaji inamtegemea sana na inaona inapewa fedha ambazo ni faida kubwa na inaweza kupata wachezaji wengine na faida juu. Basi ikubali kufanya biashara badala ya kuwa na wale viongozi wanaoangalia mashabiki watajifikiriaje au watasema nini.
Kuuza mchezaji si ujiko au maumivu. Ni biashara ya mpira ambayo inaunga mambo mengi, moja ni kuwa na wachezaji bora wanaouzika na hapa kitengo cha biashara kinafanya kazi pamoja na benchi la ufundi linalokuwa linaongozwa na Kocha Mkuu au Mkurugenzi wa Ufundi.

Thamani:
Simba lazima ikuze thamani yake kuvutia watu wengi zaidi. Lakini lazima kuwe na mipango bora ya kuvutia mashabiki kwa wingi uwanjani ili kuhakikisha inaingiza fedha nyingi kila inapocheza.
Hapa suala la utaalamu wa tiketi za msimu, timu za miezi miwili, nusu msimu na kadhalika.
Lakini kuwavutia watu kwenda angalau na familia zao, wake au wapenzi wao ni jambo ambalo linatakiwa kuendeshwa na kampeni za kitengo cha masoko.

Wadhamini sahihi:
Timu itahitaji wadhamini kama ambavyo leo SportPesa au Mo Energy. Hawa ni sahihi lakini hawatoshi. Angalau Simba inapaswa kuingiza zaidi ya Sh bilioni 3 kwa mwaka kupitia jezi zake na bukta.

Hapa ni kitengo cha masoko na benchi la ufundi vinafanya kazi pamoja katika suala la kujadili kikosi bora, kinachotakiwa kushinda kupandisha thamani na baada ya hapo suala la wao kupata masoko na kuhakikisha wadhamini wanafaidika na kinachowatangaza yaani klabu.

Hapa pia yanakuwa ni mambo ya kitaalamu na viongozi lazima wawe watu wanaotoa nafasi kwa wataalamu wao kufanya kazi na wao kusimamia mifumo badala ya kutaka kufanya kila kitu.

Viongozi bora:
Lazima wawe viongozi wanaofuata utaratibu, wanaojali usahihi wa mambo na kuangalia klabu inataka nini au timu ifanywe vipi kukuza soko au thamani ya timu na klabu yenyewe.

Hapa viongozi wanaweza hata kujadili kumnunua mchezaji ghali ambaye atakuwa na msaada uwanjani lakini thamani ya klabu na kadhalika. Hivyo ni jambo ambalo linatakiwa kujumuisha timu ya viongozi wanaoweza pia kusikiliza wataalamu wao badala ya wao tu kusikilizwa kwa kuwa tu ni viongozi.

Viongozi hawa wanatakiwa kuwa bora kwa kuwa ndiyo watakaokuwa wanashikilia usukani wa safari ya Klabu ya Simba na lazima wawe watu wenye nia moja hata kama wanatokea upande wa kwanza na wa pili.

Upande wa kwanza ni ule wa wanachama wenye asilimia 51 za umiliki na upande wa pili ni ule wa mwekezaji wenye asilimia 49 za umiliki.

Hawa lazima watatofautiana ambalo si jambo baya kwa maana ya mawazo. Na kama wana nia moja, mwisho wataelewana na kufanya mambo yao katika njia iliyo sahihi ili kupata kitu kimoja na lengo namba moja ni maendeleo ya klabu.

Simba inawategemea watakaoongoza kuwa watu wanaosimamia mabadiliko. Si wanaosimamia hisia au faida zao. Si wanaosimamia, hisia au furaha ya rafiki zao kwa kuwa Simba ni ya Tanzania na itabaki vizazi na vizazi.


5 COMMENTS:

  1. Wacha kutafuta sifa kwa kuandika the obvious. Yote uliyoandika yameshasemwa .Wacha kiki.Tafuta jipya.

    ReplyDelete
  2. Yaani watu waingize mabilioni ya pesa kwenye mabadiliko halafu wasijue nini malengo yao.Wacha kujipendekeza kila mtu anajua wewe ni mwandishi wa majungu tu.

    ReplyDelete
  3. Wewe kama nani wa kumfundisha Mohamed Mo miongoni mwa wafanya biashara bora Africa jinsi ya kufanya biashara au kusimamia taasisi kuhakikisha inakuwa ya mafanikio? Unamfundisha mtu aliepata elimu bora ya biashara na kuifanyia kazi kwa vitendo kwa mafanikio, nani alikwambia anaelima leo lazima avune leo? Simba ipo katika mikakati ya kuhalalisha timu inapata maendeleo kiuchumi na kiufanisi na hakuna shaka yeyote Mohamed Mo chini ya viongozi waliopo au watakaochaguliwa ni mtu sahii na anatosha kabisa kuingoza Simba kufikia Malengo yake yanayotarajiwa. Wenye maoni yao watoe ila pale Simba kuna watu makini wasiopenda longolongo ni kazi tu.

    ReplyDelete
    Replies
    1. kwa hakika Salim Abdallah "Try again"amedhihirisha ni mmoja wa viongozi wenye weledi na anayethubutu

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic