Kocha wa makipa wa Simba, James Kisaka ni mgonjwa na
kama utahadithiwa tu, unaweza kuona ni kawaida lakini ni mtu anayehitaji
msaada.
Sioni haya kuhamasisha Kisaka asaidiwe,
sijui kesho yangu ya yako wewe kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anajua maisha yetu
yanakwenda vipi.
Gazeti la Championi lilichukua uamuzi wa
kumsaidia Kisaka ambaye upande mmoja wa mwili wake umeshindwa kufanya kazi
vizuri. Kwanza lilizungumza na Zacharia Hanspope aliyekubali kutoa kiasi cha
fedha na Championi likatoa pia.
Baada ya hapo, picha ya watu watatu,
Mwandishi wa Championi, Khatim Naheka mimi kiongozi wake tukiwa na Wilbert
Molandi tulifika kwa Kisaka eneo la Msasani jijini Dar na kumkabidhi msaada
huo.
Lakini alisisitiza kwamba anahitaji
msaada zaidi kwa kuwa hali yake si nzuri, akatueleza gharama zilivyo kubwa na
namna ambavyo kipato chake kilivyo na imeelezwa nafasi yake ya kazi ametafutwa
mtu mwingine, Idd Pazi.
Maneno yake yalitungia na namna ya
kumsaidia ilikuwa ni kuwaeleza wadau wa michezo kuhusiana na hali ya Kisaka si
nzuri na anahitaji michango, pia tumewaonyesha sisi si maneno pekee badala yake
tumejitahidi kufanya mambo mawili, kwanza kwenda kumtembelea mgonjwa kwake
kuonyesha urafiki wetu si kazini pekee, pia tumemchangia.
Picha tukiwa na Kisaka zilizagaa
mitandaoni na nilipopitia, ajabu nikakuta mambo ambayo angalau yamenivutia leo
kulijadili suala hilo katika Metodo.
Baadhi ya watu walisema naona raha
kupiga na Kisaka kwa kuwa ni mtu maarufu, hilo halikunitikisa kwa kuwa kama ni
watu maarufu nimepiga nao picha au kufanya mahojiano ni wengi mno na wengine
wanamzidi umaarufu Kisaka tena mbali sana, haiwezi kuwa ishu.
Lakini ninachotakla kuzungumzia ni namna
baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao ninafahamiana nao walivyoonyesha si watu kwa
kulaumu eti tumemsaidia Kisaka kwa kuwa Championi ni Simba, kichekesho.
Hauwezi kutegemea kusikia mtu mwenye
akili timamu na anayeelewa maana ya ushabiki wa timu hizo mbili anaweza kusema
hivyo. Kweli, Yanga na Simba zimekuwa zikitumika vibaya na hasa kwa mashabiki
wageni, wale walioanza kuzishangilia kuanzia miaka ya 1990.
Kabla ya hapo, Yanga na Simba, mashabiki
wake waliishi kama ndugu wakisaidiana kwa hali na mali nje ya mpira, ndiyo
maana wakaitana watani wa jadi, wanataniana mpirani baada ya hapo maisha
yanaendelea.
Lakini leo Yanga na Simba wamekuwa kama
maadui, watu hawapendani kwa makusudi, wanachukiana kwa kukusudia. Kwa kuwa tu
eti wanashangilia timu tofauti, naamini wanahitaji shule, wajifunze kwa
wakongwe namna hao Simba na Yanga wa zamani walivyoishi pamoja na upendo.
Mashabiki hao wageni inabidi wasiamini
wanazijua sana Yanga na Simba wakati hawataki kujifunza, maana kama inafikia
mtu anaona mtu ni mgonjwa anasaidiwa badala ya kujadili anavyoumwa na
ikiwezekana kuhamasisha asaidiwe, analalamika kwa kuwa aliyesaidiwa
anashangilia timu tofauti, ujinga.
Maana yake, Yanga yuko tayari kumuona
Simba anapoteza maisha kwa kuwa tu si shabiki wa timu yake. Hakika Yanga
anayejitambua hawezi kufanya upuuzi huo.
Huu ni mfano tu, lakini kuna mambo mengi
sana mashabiki wageni au vijana wamekuwa wakivurunda na kuugeuza ushabiki
katika timu hizo kama uadui, si sahihi, lazima mjipange na kutafakari upya.
Ushabiki wa soka si uadui, badilikeni.
Halafu kama umeona Championi wamemsaidia
Kisaka na hawakuweza kumfikia mtu mwingine ambaye ni mwanamichezo na ana
matatizo, vizuri ni kuchukua hatua, msaidieni pia kwa kuwa tuko wengi na
tunaweza kuungana kwa kidogokidogo tulichonacho kuwasaidia wenzetu maana
hatujui leo na kesho.
Waungwana, ingawa Championi si
mamilionea, tunasaidia kwa upendo wetu kwa jamii inayotuzunguka, itikadi ya
Usimba na Uyanga, kwetu haina nafasi.
Msizitumie klabu hizo kama sehemu ya
kujenga uadui, kutengana au kubaguana. Pia labda niwachagulie mfumo wa kutumia
katika ushabiki wenu, kwamba inapofikia mnataka kufanya jambo, vizuri
mkatafakari kwanza kabla ya kulifanya. Salamu kwenu mashabiki wageni.








Jembe weka no ambayo sisi wadau wadogo tulioguswa na ugonjwa wa Kisaka Tuweze Kumchangia najua,Kila mtu akitoa kwa uwezo wake jamaa atapata matibabu ya kueleweka.Mie naamini kila mmoja wetu ni mgonjwa kama sio leo basi ni baadaye
ReplyDelete