December 10, 2013



Kocha  wa makipa wa Simba, James Kisaka ni mgonjwa na kama utahadithiwa tu, unaweza kuona ni kawaida lakini ni mtu anayehitaji msaada.

Sioni haya kuhamasisha Kisaka asaidiwe, sijui kesho yangu ya yako wewe kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anajua maisha yetu yanakwenda vipi.

Gazeti la Championi lilichukua uamuzi wa kumsaidia Kisaka ambaye upande mmoja wa mwili wake umeshindwa kufanya kazi vizuri. Kwanza lilizungumza na Zacharia Hanspope aliyekubali kutoa kiasi cha fedha na Championi likatoa pia.


Baada ya hapo, picha ya watu watatu, Mwandishi wa Championi, Khatim Naheka mimi kiongozi wake tukiwa na Wilbert Molandi tulifika kwa Kisaka eneo la Msasani jijini Dar na kumkabidhi msaada huo.


Lakini alisisitiza kwamba anahitaji msaada zaidi kwa kuwa hali yake si nzuri, akatueleza gharama zilivyo kubwa na namna ambavyo kipato chake kilivyo na imeelezwa nafasi yake ya kazi ametafutwa mtu mwingine, Idd Pazi.

Maneno yake yalitungia na namna ya kumsaidia ilikuwa ni kuwaeleza wadau wa michezo kuhusiana na hali ya Kisaka si nzuri na anahitaji michango, pia tumewaonyesha sisi si maneno pekee badala yake tumejitahidi kufanya mambo mawili, kwanza kwenda kumtembelea mgonjwa kwake kuonyesha urafiki wetu si kazini pekee, pia tumemchangia.
Picha tukiwa na Kisaka zilizagaa mitandaoni na nilipopitia, ajabu nikakuta mambo ambayo angalau yamenivutia leo kulijadili suala hilo katika Metodo.
Baadhi ya watu walisema naona raha kupiga na Kisaka kwa kuwa ni mtu maarufu, hilo halikunitikisa kwa kuwa kama ni watu maarufu nimepiga nao picha au kufanya mahojiano ni wengi mno na wengine wanamzidi umaarufu Kisaka tena mbali sana, haiwezi kuwa ishu.
Lakini ninachotakla kuzungumzia ni namna baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao ninafahamiana nao walivyoonyesha si watu kwa kulaumu eti tumemsaidia Kisaka kwa kuwa Championi ni Simba, kichekesho.
Hauwezi kutegemea kusikia mtu mwenye akili timamu na anayeelewa maana ya ushabiki wa timu hizo mbili anaweza kusema hivyo. Kweli, Yanga na Simba zimekuwa zikitumika vibaya na hasa kwa mashabiki wageni, wale walioanza kuzishangilia kuanzia miaka ya 1990.
Kabla ya hapo, Yanga na Simba, mashabiki wake waliishi kama ndugu wakisaidiana kwa hali na mali nje ya mpira, ndiyo maana wakaitana watani wa jadi, wanataniana mpirani baada ya hapo maisha yanaendelea.
Lakini leo Yanga na Simba wamekuwa kama maadui, watu hawapendani kwa makusudi, wanachukiana kwa kukusudia. Kwa kuwa tu eti wanashangilia timu tofauti, naamini wanahitaji shule, wajifunze kwa wakongwe namna hao Simba na Yanga wa zamani walivyoishi pamoja na upendo.
Mashabiki hao wageni inabidi wasiamini wanazijua sana Yanga na Simba wakati hawataki kujifunza, maana kama inafikia mtu anaona mtu ni mgonjwa anasaidiwa badala ya kujadili anavyoumwa na ikiwezekana kuhamasisha asaidiwe, analalamika kwa kuwa aliyesaidiwa anashangilia timu tofauti, ujinga.
Maana yake, Yanga yuko tayari kumuona Simba anapoteza maisha kwa kuwa tu si shabiki wa timu yake. Hakika Yanga anayejitambua hawezi kufanya upuuzi huo.
Huu ni mfano tu, lakini kuna mambo mengi sana mashabiki wageni au vijana wamekuwa wakivurunda na kuugeuza ushabiki katika timu hizo kama uadui, si sahihi, lazima mjipange na kutafakari upya. Ushabiki wa soka si uadui, badilikeni.
Halafu kama umeona Championi wamemsaidia Kisaka na hawakuweza kumfikia mtu mwingine ambaye ni mwanamichezo na ana matatizo, vizuri ni kuchukua hatua, msaidieni pia kwa kuwa tuko wengi na tunaweza kuungana kwa kidogokidogo tulichonacho kuwasaidia wenzetu maana hatujui leo na kesho.
Waungwana, ingawa Championi si mamilionea, tunasaidia kwa upendo wetu kwa jamii inayotuzunguka, itikadi ya Usimba na Uyanga, kwetu haina nafasi.
Msizitumie klabu hizo kama sehemu ya kujenga uadui, kutengana au kubaguana. Pia labda niwachagulie mfumo wa kutumia katika ushabiki wenu, kwamba inapofikia mnataka kufanya jambo, vizuri mkatafakari kwanza kabla ya kulifanya. Salamu kwenu mashabiki wageni.

1 COMMENTS:

  1. Jembe weka no ambayo sisi wadau wadogo tulioguswa na ugonjwa wa Kisaka Tuweze Kumchangia najua,Kila mtu akitoa kwa uwezo wake jamaa atapata matibabu ya kueleweka.Mie naamini kila mmoja wetu ni mgonjwa kama sio leo basi ni baadaye

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic