Baada ya kutopewa nafasi katika mchezo uliopita dhidi
ya Simba, baadhi ya wachezaji wakongwe wa Coastal Union wametoweka kambini klabuni
hapo bila taarifa wakati timu hiyo ikiwa katika maandalizi ya mchezo ujao dhidi
ya Mtibwa Sugar.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya timu hiyo kilisema
kuwa, baadhi ya wachezaji hao wakongwe wa timu hiyo, wameondoka kambini hapo
bila taarifa huku wakiwa mitaani kuendelea na mambo yao binafsi.
Chanzo hicho kilisema kuwa kambini hapo hapaeleweki
kwa sasa na hii ni baada ya vijana wa timu hiyo kupewa nafasi katika mchezo
uliopita, baada ya wakongwe wa timu hiyo kutopewa nafasi kufuatia kufanya
vibaya katika mchezo wao dhidi ya Azam FC.
“Wachezaji wakongwe asilimia kubwa ni kwamba hawapo
kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ujao, wameondoka bila taarifa na
wakijua fika kwamba Jumapili (keshokutwa) tuna mechi dhidi ya Mtibwa,” kilisema
chanzo.
Alipotafutwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal, Nassor
Bin Slum alisema kitendo cha kuwapa nafasi vijana yalikuwa ni mapendekezo
kutoka kwa mwalimu wao lakini kitendo chao cha kuondoka kambini si sahihi.
“Mapendekezo ya vijana kocha ndiye aliyeamua, kitendo
cha kuondoka kambini ni kwamba wamedhihirisha kweli hawana nidhamu, walitakiwa
kuwa kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa Jumapili, hakuna
aliyewafukuza pale, wameamua kuondoka wenyewe tu,” alisema Bin Slum.
Alipopigiwa simu Boban alisema: “Mi nipo nyumbani nafanya
mambo yangu.” Kisha akakata simu. Wakati upande wa Nyosso naye bila maelezo
mengi, alisema: “Nipo nyumbani tu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment