Kasi, uwezo anavyoonyesha kiungo mchezeshaji wa Yanga,
Hassan Dilunga, vimemfanya Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans van Der Pluijm kutamka
kuwa hamuhitaji Mnyarwanda Haruna Niyozima katika mechi zilizosalia za Ligi Kuu
Bara.
Kocha huyo mwenye kitambi cha ‘kishkaji’, ameweka wazi
msimamo wake huo mara baada ya Yanga kuifunga Tanzania Prisons mabao 5-0 juzi,
ambapo amesema Dilunga ndiye anayemhitaji na siyo Niyonzima kwa kuwa kipindi
hiki ni cha mapambano makuu.
Pluijm alisema kwamba
anafurahi kuona kijana mdogo kama Dilunga anaonyesha uwezo mkubwa, ambapo
anaamini ni kutokana na kipaji alichonacho pamoja na kuzingatia
anachomfundisha.
Kuhusu Niyonzima, kocha huyo alisema: “Unajua hawa
wachezaji wote wana vipaji na wote ni wazuri lakini kuna vitu ambavyo Dilunga
anavyo vinavyonifanya nimwanzishe katika kikosi cha kwanza kwenye mechi za hivi
karibuni na pengine zilizobakia.
“Timu inahitaji ushindi katika kila mchezo uliobaki
ili tutwae ubingwa, kwa staili anayocheza Dilunga kutokana na mechi zilizobaki,
anastahili kuanza kikosi cha kwanza, anapigana, anakaba na pia anachezesha timu
kwa ustadi mkubwa zaidi.
“Angalia kombinesheni yake na (Frank) Domayo, ni
viungo ambao wote wanacheza kwa kutegemeana, wote wanakaba pamoja na kuchezesha
timu pamoja, nafikiri hiki pia ni kigezo kingine kizuri kwa Dilunga.”
Niyonzima alikuwa na uhakika kwenye kikosi cha kwanza
kwa muda mrefu, lakini ujio wa Dilunga aliyesajiliwa akitokea Ruvu Shooting
msimu huu, umesababisha Niyonzima anayesifika kwa uchezaji wa madoido kukosa
namba.
0 COMMENTS:
Post a Comment