Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likisubiri
taarifa kutoka serikalini kuhusu thamani ya kioo cha mlango kilichovunjwa na
winga wa Simba, Ramadhan Singano ‘Messi’, Bodi ya Ligi imesema kuwa lazima Messi
akumbane na rungu jingine kutoka kwao.
Bodi hiyo imesema kuwa inataka kutoa adhabu hiyo ili
iwe kama fundisho kwa wengine kwani kilikuwa ni kitendo cha kudhamiria.
Messi alivunja kioo hicho Jumapili iliyopita baada ya
timu yake kuchezea kichapo cha bao 1-0 mbele ya Coastal Union kwenye Uwanja wa
Taifa, ambapo hasira za kufungwa akazihamishia kwenye mlango wa vyumba vya
kubadilishia nguo kwa kuupiga teke.
Ofisa Mtendaji wa Bodi la Ligi, Silas Mwakibinga
alisema licha ya mchezaji huyo kulipa fidia za kioo hicho, bodi watakaa
kuangalia ni adhabu gani atatakiwa kupewa kama onyo.
“Lilikuwa tukio ambalo kila mmoja aliliona, siyo
kusema ilikuwa bahati mbaya, hivyo baada ya mambo mengine kumalizika, suala
lake haliwezi kuachwa hivihivi, kuna adhabu nyingine itatolewa kama fundisho
kwa wote,” alisema Mwakibinga.
Tayari mchezaji huyo ameomba radhi kwa kitendo chake
kwa kile alichosema zilikuwa ni hasira za kukosa mabao ya wazi, hususan dakika
ya mwisho alipobaki na mlinda mlango wa Coastal.
0 COMMENTS:
Post a Comment