March 6, 2015


Hofu imetanda kwenye kambi ya Yanga baada ya benchi la ufundi la timu hiyo kufanya kikao kizito na wachezaji wao na kuwalisha kiapo wakihofia hujuma kutoka kwa wapinzani wao, Simba.


Hatua hiyo imekuja siku chache kabla ya Yanga kuivaa Simba katika Ligi Kuu Bara, keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Yanga kwa sasa ipo Bagamoyo wakati Simba imejichimbia Zanzibar, maalum kwa ajili ya mchezo huo.

Chanzo kutoka ndani ya wachezaji wa timu hiyo, kilisema mara baada ya kurejea nchini wakitokea Botswana kuvaana na BDF, walikutana na benchi nzima la ufundi na kuwasisitiza suala zima la rushwa.

Chanzo hicho kilisema, benchi hilo la ufundi limeshtukia kuwepo na mchezo mchafu unaopangwa na wapinzani wao, hivyo wamejipanga kuhakikisha wanakabiliana nayo.

“Kiukweli viongozi tayari wamemshtukia mbinu chafu zote zinazofanywa na wapinzani wetu, wamejua njia zote walizopanga kuzitumia.

“Tulikaa na viongozi na kila mmoja kula kiapo kuwa hataisaliti timu katika mechi dhidi ya Simba, lengo kubwa tushinde mechi hiyo ili tujiwekee mazingira mazuri ya ubingwa,” kilisema chanzo hicho.

Aidha , katika hatua nyingine, wachezaji Deogratius Munishi, Juma Abdul, Edward Charles, Rajab Zahir, Pato Ngonyani, Hassani Dilunga, Danny Mrwanda, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa, Amissi Tambwe na Simon Msuva walipewa adhabu ya kuzunguka uwanja na kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm baada ya timu yao kufungwa mabao 2-1 mazoezini, juzi.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic