Kikosi cha madaktari wanne wa kitengo maalum cha
kuchua misuli kutoka katika Kituo cha Afya cha Malindi mjini hapa, wametua kwenye
kambi ya Simba iliyopo Chukwani kwa ajili ya kazi maalum ya kuwachua misuli
wachezaji wa timu hiyo na huduma nyingine zitakazohitajika.
Madaktari hao walipelekwa kwenye kambi hiyo
ambapo wachezaji wamekuwa wakijifua kujiandaa na mechi dhidi ya Yanga
itakayopigwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Akizungumzia ujio wa madaktari hao, Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Simba, Abdul Mshagama ambaye makazi yake yapo kisiwani
hapa, alisema madaktari hao walipelekwa kambini kutokana na aina ya mazoezi
wanayofanya wachezaji pamoja na umuhimu wa mechi husika.
Akiwazungumzia madaktari hao, Daktari wa Simba,
Yasin Gembe, alikiri kufanya kazi na madaktari hao lakini alisema hawezi
kuongelea zaidi suala hilo kwa kuwa hayo ni masuala ya ndani ya kambi, hivyo si
vizuri kuweka wazi kila kitu.
“Ni kweli niko na madaktari hao lakini siwezi
kuliongelea zaidi suala hilo kwa kuwa hayo ni mambo ndani ya kambi,” alisema
Gembe.







0 COMMENTS:
Post a Comment