Na Saleh Ally
NIANZE
na pongezi kwa kikosi kizima cha timu ya taifa, Taifa Stars kwa sare ya bao 1-1
dhidi ya Uganda, The Cranes katika mechi ya kuwania kucheza michuano ya Chan
ambayo tayari tumetolewa.
Hakika
kwa hali tulitokuwa nayo, sare si jambo la kujivunia. Lakini kutokana na hali
tuliyokuwa tumefikia, hatuna ujanja zaidi ya kujipongeza kwa maana ya kuamini
mabadiliko waliyoyataka Watanzania, yana ahueni.
Kutoka
timu ya kufungwa hovyo, timu ya kuonewa hata na kila mnyonge na angalau
kuonekana ni timu inayoweza kujitutumua na kuonyesha kuwa ina makali au inaweza
kupambana.
Mechi
tano za nyuma, sema dakika 450, Stars chini ya Mzungu mwenye mbwembwe nyingi,
Mart Nooij ilikuwa haijafunga hata bao moja. Jana, ndani ya dakika 90 za
Charles Boniface Mkwasa angalau ilipata bao moja tena ikiwa imetangulia
kufunga.
Sasa
ni njia au mwanzo mzuri kuwa Stars inaweza kufunga hata kama ugenini. Unaweza
kusema Taifa Stars imeanza safari yake vizuri na kinachotakiwa kufanyika sasa
ni kuendelea kuiunga mkono.
Angalia
wachezaji walicheza katika kikosi cha juzi pale Nakivubo jijini Kampala, si
Yanga na Simba pekee. Angalia washambuliaji walioongoza mashabilizi, au mabeki
wa pembeni, si wa Yanga na Simba kama ilivyokuwa hapo awali kwa makocha wa
kigeni.
Hii
inaonyesha Charles Boniface Mkwasa na benchi lake la ufundi wanaweza kufanya
jambo kubwa na kuisaidia timu. Lakini, moja lazima tukubali wanahitaji muda.
Pamoja
na kuwaunga mkono kuanzia Mkwasa na wenzake, nimeanza kuona kuna kosa kubwa
linafanyika kupitia sehemu mbalimbali kuanzia kwenye mitandao ya kijamii,
mitaani na hata katika vyombo vya habari.
Hisia
za kwamba Mkwasa ndiye kocha sahihi, alichelewa kupewa nafasi na kwa mijadala
na mazungumzo inaonekana Mkwasa ndiye kila kitu kama vile sasa Watanzania
tumeokoka kutoka katika sehemu tuliyokuwa tumekwama.
Wako
ambao wameanza kuamini kabisa kwamba Mkwasa ndiye kila kitu na huenda matumaini
ya kuzishinda Misri na Nigeria yamerejea. Jambo hili si sahihi na tukiendelea
kulipa nafasi litatuangusha na mwisho tutarudi tena kwenye kulaumina.
Lazima
tukubaliane, Mkwasa si mtu sahihi kwa leo na kesho ya Taifa Stars. Mkwasa ni
mtu sahihi katika kipindi hiki cha kuleta mabadiliko na maendeleo na mwisho
lazima tumuunge mkono.
Kumbukeni
Mkwasa ndiyo amepewa timu hiyo ya taifa, ni mara ya kwanza kwake. Hatuwezi
kuutaja ubora kupindukia kuhusiana nay eye kama kocha bora kuliko wote na
tuamini kwamba tutafanikiwa kila kitu.
Kupewa
kwa Mkwasa, tukubali bado ni jukumu zito kwake na kuna mambo kadhaa analazimika
kuyabadilisha kwa kujaribu na kupata uhakika kwa vitendo. Lazima tukubali
unaweza usiwe wakati wa furaha kuu kwa Taifa Stars kufanya vizuri kwa kiwango
cha asilimia mia.
Lakini
kuna uwezekano kwa Taifa Stars kufanya vema tofauti na ilivyokuwa chini ya
Nooij ambaye alikuwa na maneno mengi kuliko vitendo. Tukubali kuuunga mkono
Mkwasa lakini tukubali, si mtu sahihi wa baadaye ambaye atatuvusha kila sehemu
tunayotaka.
Tunahitaji
kucheza Kombe la Mataifa Afrika, tunahitaji kuvuka hadi Kombe la Dunia.
Tunataka kuwa vinara wenye heshima kubwa Afrika Mashariki na kati, heshima
ambayo tumeipoteza kabisa na kuonekana hata Rwanda wana nafuu kuliko sisi.
Mkwasa
anaweza kututoa tulipo, lakini bado tunatakiwa kupitia sehemu zenye uwezo wa
juu zaidi hapo baadaye ili kutimiza tunachokitaka. Kingine muhimu ni lazima
Mkwasa na wenzake akina Abdallah Kibadeni, Hemed Suleiman Morocco na wengine
wakubali kupokea maoni, halafu wayafanyie kazi kwa njia zao wenyewe. Wasijisahau
Stars ikifanya vizuri mara mbili, wavimbe vichwa, wawe wasioambilika wala
kushauri. Tutarudi kulekule.
0 COMMENTS:
Post a Comment