Mshambuliaji Kpah Sherman wa Yanga, amesema msimu ujao lazima
atumie jezi namba 10, iliyokuwa ikimilikiwa na straika Jerry Tegete kwa muda
klabuni hapo, huku jezi hiyo ikimfanya Sherman kuwa mchezaji pekee
aliyebadilisha jezi mara nyingi kuliko mchezaji yeyote.
Tangu ajiunge na Yanga akitokea Cetinkaya ya Cyprus msimu
uliopita, nyota huyo ametumia jumla ya jezi nne, akifuatiwa na Amisi Tambwe
aliyebadilisha jezi mara tatu ndani ya msimu mmoja akiwa na Yanga.
Wakati anasajiliwa, Sherman alianza kwa kuvaa jezi namba 25, kisha
kubadilisha na kuvaa namba 29 kabla ya kuhamia jezi ya ‘nuksi’ namba 9 ambayo
aliitumia hadi kumalizika kwa msimu uliopita.
Sherman alisema kwa muda mrefu aliitamani
jezi namba 10, lakini ilikuwa ikitumiwa na mmoja wa wachezaji wakongwe klabuni
hapo, hivyo aliamua kutulia huku akiumia kwa kuwa anaamini ina bahati kwake.
“Namba 10 ndiyo jezi yangu, niliipenda tangu zamani, lakini
nilipofika hapa, bahati mbaya nilikuta ikitumiwa na mtu wa siku nyingi klabuni
(Tegete), hivyo sikuwa na namna.
“Ndiyo maana baada ya kusikia kwa sasa iko huru, sikutaka
kuipoteza tena, nikaiomba, naamini msimu ujao ndiyo itakuwa jezi yangu,”
alisema Mliberia huyo.
Tambwe wakati anajiunga na Yanga alianzia jezi namba 29, kisha 19
kabla ya kuchukua jezi ya Mrisho Ngassa namba 17, ambayo anasema ndiyo jezi
yake tangu aanze soka na aliitumia kila alikopitia.
0 COMMENTS:
Post a Comment