Baada ya kufanikiwa kuichezea kwa mara ya kwanza timu ya Yanga, kiungo mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Mniger Issofou Boubacar, ametamka kama akiendelea kupata nafasi ndani ya kikosi hicho, ataweza kushirikiana vyema na washambuliaji wengine waliopo ndani ya timu hiyo kama Ngoma na Tambwe na kuongeza idadi ya mabao wanayoyapata kwenye michezo yao.
Boubacar amesajiliwa kwenye usajili wa dirisha dogo akiwa sambamba na mshambuliaji, Paul Nonga ambapo wote walifanikiwa kucheza katika mchezo huo dhidi ya Mbeya City uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kushinda 3-0, juzi Jumamosi.
Boubacar amesema kuwa baada ya kusoma mazingira ya kikosi cha kwanza, sasa anajipanga zaidi kuweza kuonyesha uwezo wake pale atakapopata namba tena kwa kushirikiana na wenzake kutengeneza mabao zaidi.
“Kwanza nafurahi kuwepo katika kikosi cha Yanga, kwani ni miongoni mwa klabu kubwa kwa mchezaji yeyote yule. Hapa unapewa kila kitu ambacho unakihitaji kama mchezaji lakini pia wachezaji wake wanacheza vizuri.
“Nimeweza kuwasoma baadhi ya wachezaji na kuona viwango vyao ambapo wote wapo vizuri, hasa eneo la ushambuliaji ambapo wapo Ngoma na Tambwe ila naamini uwepo wangu utaongeza makali kwenye safu hiyo na kuifanya itambe zaidi kwa kupata mabao mengi,” alisema Boubacar.
0 COMMENTS:
Post a Comment