December 28, 2015

MAGURI

Straika nyota wa Stand United ya Shinyanga, Elias Maguri ambaye hivi karibuni alikuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo, huenda asionekane tena uwanjani baada ya kuvurugana na kocha mkuu wa timu hiyo, Mfaransa, Patrick Liewig.

Maguri ambaye kwa sasa anashika nafasi ya pili kwa kuzifumania nyavu akiwa na mabao tisa nyuma ya Mrundi wa Yanga, Amissi Tambwe mwenye mabao 10, anadaiwa kutoelewana na Liewig ambaye pia aliwahi kuwa kocha wa Simba.

Inadaiwa kuwa hali hiyo imesababishwa na mashabiki wa soka hapa nchini ambao wamekuwa wakimshangilia Maguri pindi anapokuwa akiingia uwanjani kuitumikia timu hiyo lakini pia anapoonyesha kiwango cha juu pindi anapoitumikia klabu hiyo.
LIEWIG

Hali hiyo inadaiwa kumuudhi vilivyo Liewig na kujikuta akichukua maamuzi magumu ya kumtupa benchi Maguri akidai kuwa hataki mchezaji staa kwenye kikosi chake.

Akizungumzia sula hilo Maguri alisema: “Ni kweli kabisa, maelewano yangu na kocha siyo mazuri na amekuwa akinichukia bila ya sababu za msingi.

“Hata hivyo, sababu yake kubwa iliyomfanya anichukie ni kitendo cha mashabiki kunishangilia na kulitaja jina langu pindi ninapoingia uwanjani kuitumikia timu yangu na ninapofanya vizuri.

“Nakumbuka katika mechi na Yanga, mashabiki waliponishangilia palepale alinyanyuka katika benchi na kunitoa lakini pia tulipocheza dhidi ya Ndanda alinifanyia hivyo na jana (juzi) dhidi ya Coastal Union hakunipanga kabisa.

“Nilijaribu kumuuliza kwa nini ananifanyia hivyo, akasema hataki staa katika kikosi chake, staa ni yeye tu.” 


Alipotafutwa Liewig kwa njia ya simu aligoma kulizungumzia suala hilo na kudai: “Siko tayari kusema chochote juu ya hilo, ila suala la kumpanga au kutompanga nalijua mimi ambaye ndiye kocha wake.”

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic