January 4, 2017
Benchi la Ufundi la Simba chini ya Mcameroon, Joseph Omog, limekataa kuiga mbinu zinazotimiwa na wapinzani wao wa jadi Yanga katika kusaka pointi kwenye mechi zake zote za kimashindano.

Yanga chini ya Kocha Mzambia, George Lwandamina, imekuja na mbinu mpya ya kufunga mabao mengi katika mechi moja kuhakikisha hata ikitokea bahati mbaya wamefungana pointi na wenzao, basi wao wawe juu kwa mabao.

Agizo hilo la Lwandamina lilikuja siku chache baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya African Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa takribani wiki mbili zilizopita. 

Baada ya mchezo huo, Yanga ikaichapa Ndanda mabao 4-0 kwenye ligi kuu, kisha juzi Jumatatu kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ikaikandamiza Jamhuri mabao 6-0.

Kutokana na hali hiyo, Kocha Msaidizi wa Simba, Mganda, Jackson Mayanja, akaibuka na kusema: “Soka la sasa haliangalii unafunga mabao mangapi bali kinachoangaliwa umepata pointi ngapi katika mchezo mmoja.


“Hali hiyo inatokana na mabadiliko ya kila siku ya namna ya uchezaji, ukiangalia duniani kote kwa sasa timu nyingi zinasimamisha straika mmoja mbele na si wawili kama ilivyokuwa zamani, hivyo sisi hatuwezi kuiga wenzetu wanaotumia mbinu za kufunga mabao mengi wakiamini ndiyo njia pekee ya kufikia malengo yao.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV