September 20, 2017



Na Saleh Ally
HIVI karibuni, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilipitisha majina ya wagombea wa mwisho ambao watawania nafasi za uongozi katika Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).

Uchaguzi huo wa Bodi ya Ligi umepangwa kufanyika Oktoba 15, mwaka huu ili kuwapata viongozi wapya watakaokiongoza chombo hicho muhimu katika soka.

Tunahitaji watu imara, waelewa na wenye nia ya kuuendeleza mchezo wa soka. Na Oktoba 15 watakuwa ndiyo wanapatikana ili kuanza safari ya kufanya kilicho bora ambacho kinasubiriwa kwa hamu.

Katika mchezo wa soka, baada ya ule uchaguzi mkuu wa TFF uliofanyika mjini Dodoma Agosti 12, hii ni nafasi nyingine na siku nyingine ambayo itakuwa na majibu ya safari nyingine mpya.

Nasema ni safari mpya kwa kuwa, kama utapata TFF ambayo tunaamini ni bora na Bodi ya Ligi bora, basi ninaamini kunakuwa na nafasi ya kutengeneza maendeleo ya mchezo wa soka katika njia sahihi.

Sote wala hatuna hata haja ya kupigana chenga na kuzungumza mambo mengi kuhusiana na mchezo wa soka, kwamba tumedanganywa sana, tumevurugwa sana na mliona katika uongozi wa TFF uliopita.

Uongozi uliopita umeongoza kuvuruga mchezo wa soka kwa kiasi kikubwa. Najua wakati tukieleza ukweli kulikuwa na kila namna ya hila kuonyesha wahusika wanaonewa au kuna ushabiki na kadhalika.

Lakini ukweli unaonekana, sasa viongozi karibu wote niliowalalamikia wanalalamikiwa pia. Achana na wale unaojua, wako ambao wamekumbwa na kashfa ya vyeti feki na wengine wanaonekana walikuwa katika nafasi ambazo viatu havikuwatosha.


Kusema ukweli kunaweza kuchelewa sana kuaminika, lakini ukweli ni mzuri kwa kuwa unakuwa ni akiba. Ukweli ndiyo kila kitu katika maisha ya kweli ambayo hayahitaji hila.

Ili Bodi ya Ligi ifanye vizuri lazima iwe na viongozi imara. Kwa mara nyingine ninadhubutu kusema bila ya upendeleo kwamba uongozi uliopita wa Bodi ya Ligi haukuwa madhubuti.

Uongozi uliopita chini ya Hamad Yahaya ulikuwa dhaifu, ulioshindwa kusimama katika mambo mengi ambayo yanahusika katika kuendeleza mchezo wa soka nchini.

Uongozi wa Bodi ya Ligi chini ya Yahaya uliwekwa mfukoni na TFF ya Jamal Malinzi na ukashindwa kutekeleza majukumu mengi ambayo ilionyesha wazi walistahili kuyafanyia kazi.

Mambo mengi hayakufanyiwa kazi kwa wakati mwafaka au hayakufanyiwa kabisa kazi bila ya kujali kuwa jambo fulani lilikuwa wazi kabisa au la!

Masuala ya usimamizi katika ukusanyaji takwimu za ligi, Bodi ya Ligi imekuwa hoi kabisa na watendaji wake wamekuwa wakikerwa na waandishi wanaotaka takwimu licha ya kwamba kuna watu wa takwimu ambao wanalipwa.

Utendaji wa kufuata TFF inataka nini, uliifanya Bodi ya Ligi chini ya Malinzi ionekane ni bendera fuata upepo. Kukawa hakuna tofauti ya vyombo hivyo unapozungumzia ubunifu wa mambo na utendaji bora.

Nisingependa kwenda ndani zaidi kuonekana napiga kampeni. Lakini uongozi wa Bodi ya Ligi chini ya Yahaya ulifeli na kama ingekuwa ni haki, huenda usingerudi tena.

Yahaya atagombea na Clement Sanga ambaye ni kaimu mwenyekiti wa Yanga baada ya aliyekuwa mwenyekiti kujiuzulu.

Kwa haki bila ya hofu bila kupindisha maneno, kama ningepata nafasi ya kupiga kura, basi moja kwa moja ningeiangushia kwa Sanga na si Yahaya.

Ningeiangushia kwa Sanga kwa kuwa naona ni wakati wa mabadiliko, ningeiangushia kwa Sanga kwa kuwa ninaamini ni mmoja wa viongozi bora kati ya watu niliowajua.

Sanga ni Yanga na kila mmoja anajua, lakini si shabiki, si mbaguzi, si shabiki njaa, si kiongozi mbabaisha mambo, si kiongozi mwenye tamaa.

Lakini Sanga ni kiongozi mwenye mipango, kiongozi mpenda haki, mwenye mahesabu na ambaye hawezi kubabaishwa na ushabiki ili kupindisha jambo sahihi.

Kwa viongozi wa Simba au klabu nyingine, ninaamini wanamjua Sanga. Kwa wale walio Yanga, wakiwemo wale makomandoo wapinga mizinga, ninaamini mnamjua Sanga na tabia zake.

Kwa muda ambao Yahaya amekaa madarakani na alichokifanya huenda anajua wazi kuwa alifeli. Huenda anataka njia ya kurekebisha mambo au kufanya vema. Lakini ingekuwa vizuri mapema angeamua kutoa nafasi kwa mtu kama Sanga.

Kawaida yangu sipendi kumpigia mtu kampeni. Hili la Bodi ya Ligi limenigusa na niwe mkweli, pamoja na kwamba siwezi kupiga kura nisingependa kuiona Bodi ya Ligi inarejea katika uongozi uleule ulioshindwa kuonyesha uimara wakati wa kipindi cha Malinzi.

Nisingependa kuuona uongozi ambao ulionekana ni tawi la maamuzi mabaya ya TFF iliyopita ukirejea madarakani. Hakika vema kukawa na uongozi mpya wa Bodi ya Ligi ili kuendana na kasi ya mabadiliko.

Kwangu bila ya hofu, bila ya woga wala kupindisha maneno au kuhofia lawama, nasema vema achaguliwe Sanga ili tupate watu ambao wanaweza wakaendana na mabadiliko yaliyofanyika TFF.

Yahaya ni mmoja wa watu poa sana kama utazungumzia uungwana na heshima kwa wengine. Sijawahi kusigana naye hata mara moja, wala sijawahi kusikia akilaumiwa kwamba si mtu mwema. Lakini Bodi ya Ligi, imefeli chini yake.

Nimeanzisha mjadala huu, najua huenda wengine wakaandikaa au kuzungumza kutaka kuonyesha nilikosea, nawakaribisha. Lakini nakuwa wazi bila ya kificho, nataka mabadiliko na watu wasioyumbishwa. Kura yangu kwa Sanga.



NAFASI YA MWENYEKITI:
Clement Sanga
Hamad Yahya

MAKAMU MWENYEKITI
Shani Christoms

WAJUMBE (KLABU LIGI KUU)
Hamisi Madaki
Ramadhani Mahano

WAJUMBE (KLABU DARAJA LA KWANZA)
Almasi Kasongo

WAJUMBE (KLABU DARAJA LA PILI)
Edgar Chibura.

Mazoezi hayo ya takribani saa moja yamefanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Chini ya Kocha George Lwandamina, wachezaji hao walifanya mazoezi mepedi kabla ya kuondoka na kurejea makwao.

Jana wachezaji hao waligoma kufanya mazoezi wakidai mishahara yao ya miezi miwili.

Hata hivyo, kabla ya mazoezi wachezaji walifanya kikao cha takribani dakika 17 kabla ya kukubaliana na kuanza mazoezi.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic