LIGI Kuu Tanzania Bara kwa sasa imeshaanza kutimua vumbi ambapo kila timu inapambana kutimiza majukumu yake katika kusaka pointi tatu muhimu.
Tumeona kwamba kila timu inapambana kupata matokeo na kinachopatikana kinaonekana baada ya dakika 90 kukamilika baada ya ligi kuanza kutimua vumbi Septemba 27 na ilisimama kwa muda kutokana na timu za taifa kuwa na mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia.
Ushindani umekuwa mkubwa na hali hii inatakiwa kuwa endelevu mpaka mwisho wa msimu ili kufanya kila mchezaji aone thamani ya kushiriki ligi na kucheza kwa kujituma.
Kwa wachezaji nao wana kazi ya kuonyesha kile ambacho wanacho kwenye miguu yao kwa kucheza kwa akili pamoja na nidhamu ili kutimiza malengo yao pamoja na ya timu kiujumla.
Sio kazi rahisi kufikia malengo ikiwa wachezaji watashindwa kutimiza majukumu yao kwa umakini wakishirikiana na benchi la ufundi bila kuwasahau viongozi.
Ipo wazi kwamba mwanzo kila timu huwa inakuwa na shauku ya kuonyesha kile ilicho nacho. Kwa kufanya hivyo kunaongeza ushindani na nguvu ya kila mchezaji kusaka ushindi ndani ya uwanja.
Baada ya usajili kufungwa maana yake kinachotakiwa kufanyika ni kazi ndani ya uwanja na kuacha zile porojo za wakati ule wa usajili.
Nina amini kwamba kila timu imeweka mpango kazi kwa ajili ya kufikia malengo yake. Ili kufikia malengo ni lazima kila mmoja akawa ndani ya timu jambo hili litasaidia kufanikisha mipango kwa wakati.
Tukiachana na hayo sasa hebu tutazame sehemu muhimu ambayo inahusika kutoa ushindi kwa wachezaji wawapo kazini kusaka pointi tatu ambapo ni ndani ya uwanja.
Ubora wa uwanja hasa sehemu ya kuchezea ni muhimu kuwa bora wakati wote ili kutoa burudani kwa wale ambao wanacheza pamoja na mashabiki ambao wanajitokeza kuona burudani.
Ukweli ni kwamba wengi huwa wanatazama sehemu ya kukaa mashabiki pamoja na sehemu ya kubadilishia nguo na kuachana na habari za sehemu ya kuchezea.
Katika hili hapa ninaona kwamba ni makosa ambayo yanafanyika kwa sababu ambazo ninashindwa kuzielewa lakini nina amini kwamba ikifanyiwa kazi kwa ukaribu majibu yatapatikana.
Ikiwa ni mwanzo wa ligi basi ni muhimu kwa sehemu ya kuchezea kuwa bora na kutunzwa ili iweze kuwa rafiki kwa wachezaji pamoja na kutoa matokeo mazuri ndani ya uwanja.
Tumeona kwamba mwanzo wa ligi Uwanja wa Ushirika Moshi ulishindwa kutumika kwa ajili ya mchezo ule wa awali kati ya Polisi Tanzania v KMC na ulipelekwa Uwanja wa Karatu kutokana na suala la ubora.
Muhimu kuwa na sehemu nzuri ya kuchezea ili kuwapa nafasi wachezaji kuonyesha ule uwezo wao kwa kuwa imekuwa ni tatizo la muda wote hasa kwenye suala la viwanja bado mambo yamekuwa ni magumu.
Matokeo ndani ya uwanja yanapatikana ikiwa sehemu ya kuchezea itakuwa bora na kila mmoja atacheza kwa kujiamini tofauti na viwanja vingine ambavyo havikuwa bora.
Ikiwa viwanja vingine vipo na havina ubora ninashauri vifanyiwe maboresho na yakitokea haya mafanikio makubwa yataonekana hapo baadaye.
Tumekuwa tukilalamika kwa muda mrefu kuhusu viwanja na ubora wa sehemu za kuchezea kwa baadhi ya sehemu ambazo zimekuwa zikilalamikiwa mara kwa mara.
Muda mwingi kuhusu sehemu ya kuchezea wengi wamekuwa wakitazama na kuboresha sehemu za kukaa mashabiki pamoja na vyumba vya kubadilishia nguo.
Watu kuwekeza nguvu kubwa sehemu ya kukaa halafu sehemu ya pitch kuiweka kiporo inaumiza hasa kwa wale ambao wanaingia uwanjani kusaka ushindi basi ni wakati wa kuboresha na viwanja ili kuongeza ushindani.
0 COMMENTS:
Post a Comment