SITAKI
kabisa kuingia kwenye mkumbo wa kuwalaumu vijana walio kwenye kikosi cha Taifa
Stars maboresho wala kocha wao Salum Mayanga.
Kamwe
sitawaunga mkono watu waliokuwa wanawazomea pale Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam juzi wakati walipocheza na kufungwa mabao 3-0 na wageni wao Burundi huku
Amissi Tambwe na Didier Kavumbagu wakifunga bao moja kila mmoja.
Kweli
inauma kwa kuwa timu ya taifa ni yangu mimi, wewe na Watanzania wote. Sasa vipi
ifanyiwe mzaha kama ambao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanaona ni kitu rahisi
na inawezekana tu kufanyika?
Sina nia ya
kupinga wanachokifanya kuhusiana na kuwatafuta vijana mikoani, kuwaweka kambini
na mwisho kufanya mchujo wa kuwapata wale ambao wameunganishwa kwenye kikosi
cha timu ya taifa na jana kwa mara ya kwanza wakapewa nafasi ya kucheza kwenye
kikosi cha kwanza cha Taifa Stars!
Ukiwaona
wale vijana wanacheza, utakubaliana nami kwamba kweli wana vipaji, ni sehemu ya
vipaji vya wachezaji wengi wa Kitanzania ambavyo hupotelea mitaani, hivyo ni
jambo zuri kuvitafuta na kuanza kuvionyesha.
Lakini
nasema huo ni mzaha na hasa mambo yanavyopelekwa, haiwezekani na haitawezekana
rundo la wachezaji kutoka katika timu za daraja la tatu au zile za mchangani
wapewe mafunzo halafu moja kwa moja wanakwenda kuichezea timu ya taifa
inayocheza dhidi ya taifa jingine, huu ni mzaha!
Wachezaji
ambao hawajacheza hata mechi moja ya ligi, wachezaji ambao hawajui mikikimikiki
ya michuano ya kimataifa, wanapewa nafasi ya kuanza kuichezea timu ya
taifa. Ninaamini kuna utani na TFF ya
sasa, TFF chini ya Jamal Malinzi, kiasi fulani hawajui maana ya timu ya taifa.
Vijana
waliowateua kweli ni wazuri, lakini bado kuna sehemu wanatakiwa wapite ili
kufikia hatua ya kuichezea timu ya taifa. Kama kweli sisi tunaishi dunia hii
ambayo kuna mataifa mahiri ya soka kama Brazil, Uholanzi, Hispania, Ivory
Coast, Ghana na mengineyo, vipi tunakuja na mfumo wetu pekee ambao hakuna
anayeweza kuufanya?
Timu ya
taifa ni ‘cream’ ya taifa. Wachezaji bora kabisa kwenye nchi, hilo ndilo
ninalojua. Sasa TFF wanaweza kusema vijana hao ndiyo bora zaidi kwa nchi hii!
Kawaida wachezaji walio na sifa hiyo hupatikana kutokana na ligi ya nyumbani na
zile za nchi nyingine.
Tambwe na
Kavumbagu wamepata nafasi ya kucheza kwenye timu yao ya taifa kwa kuwa
wanacheza ligi ya Tanzania Bara na wanafanya vizuri katika timu zao. Hao
waliochezea Taifa Stars wanafanya vizuri wapi? Sasa kigezo cha kupata nafasi
hiyo ni kipi? Au utaratibu upi umetumika?
Uzoefu wao hadi
kufikia hapo ni upi, vipi wapewe nafasi ya kuichezea Taifa Stars? Si sahihi na
timu hiyo si ya kufanyia majaribio ya wachezaji tena katika mechi ambayo
inaingia kwenye rekodi kuwa Stars ilicheza mechi ngapi, ikashinda ngapi,
ikapoteza na sare ngapi. TFF mnalijua hili? Au ndiyo ilimradi bora twende na
kwa kuwa mna washauri wenu wa kuunda timu ambao wanaamua mambo ilimradi tu!
Ndiyo maana
nasema Kocha Salum Mayanga na wale vijana hawana kosa lolote, hili ni tatizo la
TFF ambayo kama imefanya kitu lakini inaonekana ina haraka sana na inataka
vijana wale waonekane tu ili ijulikane imefanya kazi. Huenda ni kutaka
kuwaridhisha wadhamini wao, kitu ambacho si sahihi.
Angalia
kuna mchezaji mmoja aliingizwa katika kipindi cha pili, ni mshambuliaji. Wakati
timu inapambana kusawazisha, angalau kupata bao moja ikiwa imefungwa tatu, yeye
alikuwa akiupoza mpira na baadaye kupiga visigino, mashabiki wakaanza kumzomea.
Maana alionyesha anavyojali furaha yake kuliko umuhimu wa taifa.
Lazima TFF
wakae na kulifanyia kazi hilo, kama wataendelea hivi hata huyo kocha mpya
Mholanzi atakuwa hana maana kwa kuwa atapotea njia.
Lakini ukiachana
na wachezaji, jamani hebu angalieni jezi ambazo Taifa Stars walivaa kwenye
mchezo ule, hazikuwa na uhalisia wowote kuwa inayocheza ni timu ya taifa.
Kwanza
zilikuwa na kiwango duni, lakini pia hazikuwa na rangi zetu ambazo tumezizoea
kwenye timu ya taifa pamoja na kwamba ilikuwa siku maalum ya Miaka 50 ya
Muungano.
Taifa Stars
si sehemu ya majaribio, nafikiri mmeelewa. Nitarudi siku nyingine.
Fin.
0 COMMENTS:
Post a Comment