May 30, 2016


Na Saleh Ally
KWANZA anza kwa kujiuliza kama ungekuwa wewe ndiye Kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone ungejisikiaje? Hakika ni maumivu makali ya moyo.

Lazima ungehisi au kuamini hauna bahati hata kidogo na hasa linapofikia suala la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ndani ya miaka mitatu, Simeone amekiongoza kikosi chake kucheza fainali mara mbili dhidi ya timu moja.

Fainali ya kwanza msimu wa 2013/14 ilikuwa dhidi ya Real Madrid kama ile ya 2015/16.  Zote mbili wamepoteza, moja wakianza kufunga Madrid wakasawazisha, ya usiku wa kuamkia jana wakaanza kufungwa, wakasawazisha na kung’olewa kwa mikwaju ya penalti 5-3.

Mtu asiye na bahati kwa Lugha ya Kihispania anaitwa sin suerte. Unaweza ukampa jina hili Simeone raia wa Argentina anayeonekana ni mtu asiyekata tamaa na kila kitu.

Simeone ni kocha aliyeshinda makombe kadhaa makubwa na muhimu akiwa na Atletico Madrid. Amechukua ubingwa wa La Liga, Copa del Rey, Super Cup Hispania, Europa Cup na Uefa Super  Cup pia.
Si mgeni wa makombe tokea akiwa mchezaji hadi kocha. Lakini kombe pekee ambalo linaonekana kumteleza kila anapojaribu ni lile la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Rekodi yake na kikosi cha Atletico Madrid inamfanya aonekane mmoja wa makocha bora kabisa kuwahi kuifundisha timu hiyo aliyowahi kuichezea pia.

Tokea ajiunge nayo mwaka 2011, ameiongoza katika mechi 260. Ameshinda 164, sare 52 na kapoteza 44, hii inamfanya awe na wastani wa juu kabisa wa 63.1% ya ushindi. Huu ni wastani wa juu kwa kocha anayefundisha timu kubwa zinazoshiriki michuano yenye ushindani wa juu.


Ukiachana na rekodi za mafanikio yanayopatikana baada ya mchezo, angalia mchezo wenyewe. Mfano, fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Madrid pale jijini Milan, Italia.

Kikosi chake kilicheza vema zaidi, ingawa mwenyewe mwisho alisisitiza kwamba kuna mambo walizidiwa ambayo ndiyo yalifanya wapinzani wao mwisho wabebe ubingwa huo mbele yao.

Simeone anakubali kuwa ana maumivu ya moyo, huenda maumivu hayo yametambaa kwa mashabiki wengi wa soka duniani kote wakiwemo wale ambao si mashabiki wa Atletico Madrid, lakini wanaumia kwa kuwa wanajua kocha huyo Muargentina anaifanya kazi yake kwa ufasaha.

Wanajua kikosi chake kufikia kucheza namna hiyo ni mtu anayejituma, anayefanya jambo kwa juhudi kubwa lakini inaonekana mafanikio yanamkimbia hasa katika Ligi ya Mabingwa.

Kabla ya mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa jijini Milan, Ronaldo de Lima alipata nafasi ya kumzumngumzia Simeone ambaye alicheza naye timu moja wakiwa Inter Milan ya Italia pia.

Ronaldo alianza kwa kupinga tabia ya Simeone kupandikiza hasira za Kiargentina kwa wachezaji wake, akisema wanakuwa wajeuri na wakatili. Lakini mwisho, akasema ni wagumu kushindika na kocha huyo ni kati ya makocha bora kabisa duniani. 


Kwenye kutengeneza jambo mengi yanatokea, lakini mwisho ni matokeo bora. Simeone amekuwa akiyapata lakini tatizo kubwa ni Ligi ya Mabingwa.

Kinachovutia kwa huyu jamaa ni maneno yake ya mwisho kuhusiana na kuonekana hana bahati ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Sitaki kuonyesha machungu yangu kwenu, lakini najua naumia kiasi gani kufika hapa mara mbili lakini sijarudi nyumbani na kombe. Hakuna ambaye angeweza kufurahia.

“Utaona, wachezaji wamepambana hadi mwisho, wamecheza mechi nyingi sana ndiyo maana dakika 15 za dakika 30 za nyongeza, kila mmoja alionekana ameisha kabisa.

“Najua hatukufika hapa kwa bahati hata kama kweli tuna bahati mbaya. Hatuwezi kuishia hapa, niwaahidi ninabaki Atletico na kwa mara nyingine tunataka kufika fainali ili tuiondoe bahati mbaya,” anasema.

Wengi wanaamini Atletico au Simeone wana bahati mbaya na kombe hilo. Kutokana na wanavyojituma watu wanawaonea huruma, vyote viwili anavikataa.

Utagundua kuwa Simeone si mpiganaji wa muda mfupi, si muoga, si anayetaka kuonewa huruma na anachoamini ni kurejea na kupigana tena ili wafike fainali kumaliza makosa ya fainali mbili zilizopita.

Hakuna ubishi, siku wakifanikiwa kuingia fainali tena, kutwaa kombe hilo halitakuwa na mjadala. Lakini utaona namna kamanda anavyopaswa kuwa, hata kama kaumia anaonyesha bado mapambano yanaendelea.

Simeone anaficha maumivu yake ili kuinua mioyo ya wachezaji wake lakini pia anafuta hisia za wao hawana bahati na Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya. 

Kama yeye akikubali, maana yake vijana wake wakati mwingine watakuwa hawana sababu ya kulipigania.

Hii ni falsafa ya kiongozi sahihi ambaye maisha yake yote hachoki kupambana na hakati tamaa kwa kuwa hataki kuonewa huruma. Kuhurumiwa ni falsafa ya kusaidiwa au kubebwa, Simeone hataki na tayari amerejea tena kwenye mapambano.


MAFANIKIO YA SIMEONE
AKIWA MCHEZAJI 
Atletico Madrid
La Liga (1): 1995–96
Copa del Rey (1): 1995–96

Inter Milan 
Uefa Cup (1): 1997–98

Lazio (4)
Serie A (1): 1999–2000
Coppa Italia (1): 1999–2000
Supercoppa Italiana (1): 2000
UEFA Super Cup (1): 1999

TIMU YA TAIFA
Argentina (4)
Kombe la Mabara Fifa (1): 1992
Copa America (2): 1991, 1993
Artemio Franchi (1): 1993
Medali ya Fedha Olimpiki (1): 1996

KAMA KOCHA
Estudiantes de La Plata (1)
Ubingwa Argentina (1): Torneo Apertura 2006

River Plate (1)
Ubingwa Argentina (1): Torneo Clausura 2008

Atletico Madrid (5)
La Liga (1): 2013–14
Copa del Rey (1): 2012–13
Supercopa de Espana (1): 2014
UEFA Europa League (1): 2011–12
UEFA Super Cup (1): 2012

BINAFSI 
Kocha Bora wa Mwaka La Liga (2): 2012–13, 2013–14
Tuzo ya Miguel Munoz (1): 2013–14
Kocha Bora wa Mwezi La Liga (2): Oktoba 2013, Novemba 2015




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic